Michuano ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) wakati inaanzishwa rasmi mwaka 1964-1965, timu za Afrika Magharibi na zile za Kati ndizo zilizotawala michuano hiyo kwa misimu minne mfululizo.

Timu za ukanda huo zilikuwa zikijibebea taji la michuano hiyo kwa kupokezana kabla ya ukanda wa Afrika Kaskaini maarufu kama Waarabu kupindua meza na kujitengenezea ufalme wa michuano hiyo zikianza na taji la kwanza la mwaka 1969 baada ya Ismaily ya Misri kuwa timu ya kwanza ya ukanda wa Kaskazini kubeba taji hilo kwa kuipasua TP Mazembe, kisha zikarudi kuhenyeka hadi 1976 pale MC Alger ilipozikomboa timu za Kiarabu kwa kuipiga Hafia ya Guinea. Kisha timu hizo zikaendelea kusota hadi mwaka 1981 JS Kabylie ya Algeria ilipotwaa pia taji hilo kisha timu za ukanda wa Kaskazini zikashika hatamu kwa kutamba kwenye michuano hiyo, huku Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) zikiweka rekodi ya kufika fainali ya michuano hiyo tu bila kubeba taji.

Simba FC ya Uganda, ilikuwa klabu ya kwanza ya ukanda huu kucheza fainali ya michuano hiyo mwaka 1972, kisha ikafuata Al Hilal ya Sudan mwaka 1987 iliyofanya hivyo tena 1992, huku SC Villa ya Uganda ikicheza hatua hiyo 1991 ikiwa timu ya mwisho ya Cecafa kufika hatua hiyo.

Kwa upande wa timu za Kusini mwa Afrika (Cosafa) wao walitangulia Nkana Red Devils ya Zambia kufika fainali mwaka 1990, kabla ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini kupindua meza kwa kubeba taji mwaka 1995 na mwaka 1998 baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubadilisha mfumo wa Klabu Bingwa kuwa Ligi ya Mabingwa, Dynamos ya Zimbabwe ikifika pia fainali na kufa mbele Asec Mimosas. Ukanda wa Kusini ukitulia kwa misimu michache kabla ya Mamelodi Sundowns kutinga fainali 2001 lakini ikapoteza kwa Al Ahly.

Miaka 12 baadaye, yaani 2013 Orlando ilifika tena fainali na kufungwa na Al Ahly na miaka minne baadaye Mamelodi ikafanya kweli kwa kubeba taji mwaka 2016 kwa kuichapa Zamalek ya Misri na timu ya mwisho kwa ukanda wa Kusini kufika fainali za Ligi ya Mabingwa ni Kaizer Chiefs ya Sauzi 2020-2021 japo haikubeba taji mbele Al Ahly.

Kulingana na rekodi zilizopo ni kwamba ukanda wa Kaskazini ndio wababe wa taji la michuano hiyo yua Ligi ya Mabingwa, kwa kutwaa jumla ya mataji 35, ikifuatiwa na Ukanda wa Magharibi na Kati uliobeba mataji 20, huku Kusini ikinyakua mara mbili na Afrika Mashariki ikiwa haina chao.

Hakuna ubishi ukiachana na kupindua meza, lakini timu za Kaskazini zimekuwa zikizitetemesha timu za ukanda mwingine kwa muda mrefu kwa kugawa vipigo vinono kwa baadhi ya timu hasa za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kuna kipindi ilifikia hatua timu za Afrika Mashariki zilikuwa zinachukia kupangwa na timu za Kaskazini kutokana na dozi zilizokuwa zikitolewa kwa timu za kanda nyingine zikiwamo kutoka Tanzania.

Hata hivyo, kwa kipindi cha hivi karibuni mambo yamebadilika hasa baada ya klabu za Afrika Mashariki kuamua kuwekeza na kutumia fedha kusajili wachezaji wa viwango na makocha hodari, japo ni kweli bado hazijafikia zilipo timu za Kaskazini zinanonukia utajiri wa kutisha. Ndio maana kwa sasa sio ajabu kuona Yanga imefika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuifunga USM Alger ikiwa kwao, ama Simba kwenda kuidindia Al Ahly au Wydad kwenye ardhi ya nyumbani kwao.

klabu za kanda nyingine haziogopi tena kucheza na timu za Kaskazini ndio maana imeshuhudiwa leo Mamelodi, Orlando, Petro Luanda, Nkana, Zesco na timu nyingine zikivichachafya vigogo vya Kaskazini, hata kama bado hazijaweza kuwapora ufalme wao wa kubeba mataji michuanoni.

Wachezaji wa timu za Tanzania na mataifa mengine wanazichukulia timu za Kiarabu kama timu nyingine na hakuna tena ile presha na uoga kama ilivyokuwa miaka ya 1980 hadi 2000. Utabisha nini wakati Simba mwaka 2003 iliwavua ubingwa Zamalek kwa mikwaju ya penalti baada ya kuifunga nyumbani Dar es Salaam bao 1-0 kisha kwenda kulala 1-0, huku kwa vipindi tofauti timu hiyo imekuwa ikizitambia timu za Kiarabu Kwa Mkapa.

Yanga nayo tangu ilipojikomboa kwenye minyororo ya unyonge wa miaka 32 ilipoitungua Al Ahly, leo inaweza kusimama na timu yoyote ya Kaskazini na kupimana nayo ubavu tofauti na ilivyokuwa ikipigwa mabao 4-0 au 5-0 na timu za ukanda huo kulingana na rekodi zilizopo.

Hata hivyo, ni kweli bado timu za kanda nyingine zina kazi za kupindua meza kwa timu hizo za Kaskazini, kwani zinaendelea kutawala kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa, kama ilivyo kwa Kombe la Shirikisho hasa wakati huu mechi za makundi zikiwa zimeanza.

Katika timu 16 zilizotinga hatua hiyo kwa Ligi ya Mabingwa, Kaskazini zinawakilishwa na timu sita, huku Mashariki na Kati zikiwa na timu tatu sawa na Kusini na Afrika ya Kati na Maghariki zikiwa na tỉmu nne tu.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement