Kiungo wa zamani wa Arsenal, Thomas Partey, amekana mashtaka matano ya ubakaji na moja la unyanyasaji wa kingono katika Mahakama ya Southwark Crown.


Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 anatuhumiwa kuwabaka wanawake wawili na kumnyanyasa kingono mwanamke wa tatu, matukio yanayodaiwa kutokea kati ya mwaka 2021 na 2022 wakati akiichezea Arsenal.


Katika kikao kifupi cha dakika 14 kilichofanyika Jumatano, Partey alizungumza tu kuthibitisha jina lake, tarehe ya kuzaliwa na kujibu kwamba siyo mkosaji. Kiungo huyo wa Kimataifa wa Ghana, ambaye sasa anachezea klabu ya Villarreal ya Hispania, atakabiliwa na kesi chini ya Jaji wa Mahakama Kuu mnamo Novemba 2, 2026 katika mahakama hiyo hiyo.


Partey alikamatwa kwa mara ya kwanza Julai 2022, ingawa hakutajwa jina wakati huo na aliendelea kucheza Arsenal wakati uchunguzi ukiendelea hadi mkataba wake ulipoisha Juni mwishoni. Siku chache baadaye, mnamo Julai 4, alifunguliwa mashtaka rasmi.


Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, alisema Julai kwamba alikuwa na “uhakika kwa asilimia 100” kuwa klabu ilifuata taratibu zote sahihi kuhusiana na kukamatwa na uchunguzi wa mchezaji huyo. Msemaji wa Arsenal aliongeza: “Mkataba wa mchezaji ulimalizika Juni 30. Kutokana na mwenendo wa kesi, klabu haiwezi kutoa maoni yoyote.”


Kufika kwake mahakamani kulikuja siku moja baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa ambapo Villarreal ilicheza na Tottenham Hotspur jijini London.


Jaji Christopher Hehir alimhakikishia Partey kwamba kesi yake itafanyika Novemba 2, 2026, akibainisha kuwa kuna msongamano mkubwa wa kesi kwenye mahakama za taji na washitakiwa waliopo rumande wanapewa kipaumbele.


Partey amepewa dhamana kwa masharti yale yale aliyopewa awali: kutokuwasiliana na wanawake watatu wanaodaiwa kuhusika, na kutoa taarifa polisi kuhusu mabadiliko yoyote ya makazi ya kudumu au safari za kimataifa.


Partey, ambaye awali aliishi Potters Bar, Hertfordshire, alijiunga na Arsenal akitokea Atlético Madrid mwaka 2020 kwa ada ya uhamisho ya £45m (TZS 153.1 bilioni). Aliichezea Arsenal michezo 35 ya Premier League msimu uliopita na kufunga mabao manne. Aidha, amewahi kuichezea Ghana zaidi ya mara 50, ikiwemo kwenye Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement