NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma maarufu Mwana FA amesema Tamasha la Kitaifa la Utamaduni litakuwa la kihistoria na litakusanya tamaduni kutoka mikoa yote Tanzania.

Tamasha hilo la siku saba litakalofanyika katika viwanja vya Maji Maji Ruvuma kuanzia Julai 20 hadi 27, 2024 linatarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo Juni 20, 2024 Naibu Waziri Mwinjuma amesema tamasha hilo linatokana na maagizo ya Rais Samia aliyotoa mwaka 2021 akiwa Mwanza.

“Rais aliagiza kufanyika kwa tamasha la Utamaduni kila mwaka ili kurithisha Mila na Utamaduni wa kitanzania...,

Tanzania ina utajiri wa makabila zaidi ya 120, tofauti yake inajenga Umoja na yanaunganishwa na Lugha ya Kiswahili.” Amesema Mwana FA.

“Kudumu kwa Utamaduni inategemea namna inavyorithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine na kwamba urithi wa Utamaduni ni kivutio kikubwa cha utalii, watalii wamevutiwa sana,” amesema Mhe. Mwana FA

Amesema tamasha hilo litakuwa tofauti na matamasha mengine mawili yaliyowahi kufanyika mwaka 2022 na 2023 kwani litakuwa na sura ya Kitaifa na litakuwa chini ya wizara husika.

Naibu Waziri Mwinjuma ameongeza kusema kuwa jukumu la rasilimali fedha litakuwa chini ya Sekta Binafsi ambayo ni Kampuni ya DrumBeat Carnival (Tz) Limited itakayosaidia pia kuhamasisha tamasha liwe na hadhi.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement