SVEN, NABI NA BENCHIKHA SIMBA WAWATOLEA MACHO
Licha ya makocha wengi kutoka ndani na nje ya Afrika kutuma wasifu wao kwa Simba wakitaka kazi, lakini vigogo wa timu hiyo wameyajadili zaidi majina ya makocha watatu Mtunisia Nasreddine Nabi aliyekuwa Yanga msimu uliopita, Mbeligiji Sven Vandenbroeck aliyewahi kuinoa timu hiyo na Mualgeria Abdelhak Benchikha aliyetwaa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akiwa na USM Alger akiinyang'anya Yanga tonge mdomoni. Na wameanza kutamba chinichini kwamba kiboko Yanga anakuja.
kati ya makocha watatu hao, mtu ambaye Simba inaweza kumpata kwa uharaka na rahisi ni Benchikha kuliko ilivyo kwa Sven na Nabi.
Habari za ndani zinasema kwamba, Sven ni miongoni mwa makocha walioingia tatu bora ya waalimu wanaotakiwa, lakini kuna baadhi ya viongozi wamemkataa kutokana na misamamo yake huku wengine waliwahi kukwaruzana naye kipindi yupo kikosini hapo kuanzia Disemba 2019 hadi Januari 2021, wanaamini akirejea hawataelewana vyenma.
Sven wakati anazungumza na mtandao wa iDiski Times wa Afrika Kusini, licha ya kusema yupo tayari kurejea Msimbazi lakini zaidi alionyesha kutovutiwa na mazingira ya Simba na soka la Tanzania kwa ujumla kuliko ilivyo kwa Afrika Kusini aliko na ofa pia. "Naijua Klabu (Simba) na mazingira yake, Ligi ya Afrika Kusini ni kubwa na miundombinu yao ni mizuri zaidi," alisema Sven.
Kwa upande wa Nabi, Simba ni kama imevuta pumzi na kuamua kuachana naye kutokana na kile kinachoelezwa kocha huyo anahitaji vitu vingi ikiwemo kupunguza wachezaji karibu wanane na kusajili wapya pia kupewa muda kwani anaamini Simba inahitaji muda na maamuzi magumu ili kufikia malengo.
Hali hiyo ya Sven na Nabi, imeifanya meza ya Simba kusaliwa na faili moja tu la Benchikha lakini naye pia bado viongozi wanaamini licha ya msimu uliopita kupata matokeo chanya akibeba Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na African Super Cup, lakini aina ya soka lake halitofautiani zaidi na la Robertinho aliyeondoka.
Benchikha mwenye uzoefu wa kutosha na soka la Afrika akifundisha tangu mwaka 2001, mara nyingi ameonekana kuwa kocha mwenye asili ya kujilinda na kutumia mfumo wa mabeki wanne, viungo wa chini wawili, wajuu wa tatu na mshambuliaji mmoja (4-2-3-1) kama ilivyokuwa kwa Robertinho jambo linalowapa kigugumizi baadhi ya wafanya maamuzi wa Simba.
Hata hivyo pamoja vigogo wa Simba kutopitisha moja kwa moja jina la Benchikha, na kuamua kupitia wasifu wa makocha wengine lakini Muargeria huyo bado ana nafasi kubwa ya kupewa kibarua kuliko ilivyo kwa Nabi na Sven ambao walitajwa hapo awali.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema harakati za kumpata kocha mpya zinaendelea na atatangazwa siku si nyingi. "Tutaleta kocha anayefaa kuifundisha Simba, tuna majina tayari na tunaendelea na mchakato wa kuchambua na kuamua nani tumpe timu yetu kutokana na matakwa yetu na tutawatangazia," alisema Ahmed huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Imani Kajula akijibu kwa ufupi akisema; "Tupo katika hatua za mwisho kumpata kocha mpya."
Simba kwa sasa ipo chini ya kocha wa makipa Mhispanyola Dani Cadena ambaye pia ana sifa zote za kuwa kocha mkuu, akisaidiana na nguli wa timu hiyo, Seleman Matola wakiendelea na maandalizi ya mechi ijayo, hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas Novemba 25, kwa Mkapa.