Timu ya Azam FC imesogea hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kulazimishwa suluhu na Tabora United.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, imeifanya Azam kushika nafasi ya pili na pointi 36, sawa na Simba japo kikosi hicho cha matajiri wa jiji la Dar es Salaam kimezidi mchezo mmoja na kinaongoza kwa mabao ya kufunga.

Mchezo huo ni wa 16 kwa Azam ambapo kati ya hiyo imeshinda 11, sare mitatu na kupoteza miwili huku kwa upande wa Tabora ikisalia nafasi ya 13 katika msimamo na pointi zake 17 baada ya kushinda mitatu, sare minane na kupoteza mitano.

Mechi hii ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kutokana na kilichotokea mara ya mwisho timu hizo zilipokutana Agosti 16, mwaka jana ambapo Tabora ilifungwa mabao 4-0, huku mechi hiyo ikichezwa dakika 18 tu tofauti na ilivyokuwa kawaida 90.

Matokeo hayo yanaifanya Tabora kufikisha michezo sita mfululizo bila ushindi tangu mara ya mwisho iliposhinda mabao 2-1, dhidi ya Mtibwa Sugar, Desemba Mosi mwaka jana huku kwa upande wa Azam imefikisha mechi ya tisa mfululizo bila kupoteza.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement