STARS YAPATA USHINDI WA KWANZA FIFA SERIES 2024
MABAO ya Kelvin John, Abdul Suleiman 'Sopu' na Novatus Dismas yametosha kwa timu ya taifa 'Taifa Stars' kuibuka na ushindi wake wa kwanza kwenye FIFA Series 2024 dhidi ya Mongolia huko Azerbaijan ambako waliweka kambi katika kipindi hiki cha michezo ya kimataifa ya kalenda ya FIFA.
Kelvin ambaye alikosekana kwa kipindi kirefu kwenye kikosi hicho cha Taifa Stars, amerejea na bao huku akiwa na jezi namba 10 ambayo imezoeleka kuvaliwa na nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta ambaye aliomba kutoitwa.
Mshambuliaji huyo wa KRC Genk ambaye aliongoza safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars kwenye mchezo huo, alifungua akaunti ya mabao kwa Tanzania mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya pasi nzuri kutoka kwa Ben Starkie katika dakika ya 49.
Dakika ya 62, Stars ilijipatia bao la pili ambalo lilifungwa na Sopu baada ya pasi ya mwisho iliyopigwa na mchezaji mwenzake wa Azam FC, Feisal Salum na mabao hayo yalionekana kuimaliza nguvu Mongolia ambayo inashika nafasi ya 190 kwenye viwango vya ubora wa soka vinavyotolewa na FIFA. Stars iko nafasi ya 119.
Katika dakika ya 76, Novatus Dismas ambaye alipoteza nafasi moja ya wazi alipopiga mpira nje akiwa jirani na lango, aliiandikia Stars bao la tatu baada ya kazi nzuri ya Sopu ambaye alionekana kuwa mwiba kwenye ngome ya Mongolia.
Kwa matokeo hayo, Stars imemaliza kwa kishindo michezo yake ya FIFA Series 2024 kwa kipindi hiki baada ya kuanza vibaya kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Bulgaria huko Azerbaijan.