Timu za Singida Fountain Gate na Mashujaa FC zimegawana pointi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao umemalizika kwa suluhu (0-0) katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mchezo huo ambao umepigwa leo Aprili 21, 2024 kuanzia saa 10:00 jioni, ni wa pili msimu huu kwa timu hizo kukutana ambapo mchezo wa mzunguko wa kwanza ulipigwa Novemba 6, 2023 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Singida FG ikishinda mabao 3-1.

Suluhu hiyo ni ya pili mfululizo kwa timu zote mbili, ambapo mechi zilizopita Singida FG ilipata sare ya 1-1 mbele ya Ihefu huku Mashujaa ikitoka suluhu (0-0) na Azam FC.

Kwa matokeo hayo, Singida FG inafikisha alama 26 katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi, ikipoteza mechi 10, sare nane na kushinda sita, huku Mashujaa ikifikisha pointi 23 kwenye nafasi ya 14 ikipoteza mechi 11, sare nane na kushinda tano.




You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement