Simba SC imeshinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Pazia la ufungaji kwenye mchezo huo lilifunguliwa na kiungo Sadio Kanute dakika ya 63 na kumfanya kiungo huyo raia wa Mali kufikisha mabao manne kwenye ligi msimu huu.

Kiungo raia wa DR Congo, Fabrice Ngoma akatupia bao la pili dakika ya 77 ambapo kwake ni bao la tatu msimu huu ndani ya ligi hiyo, huku jahazi la Azam likazamishwa zaidi na beki wa kulia wa Simba, David Kameta ‘Duchu’ baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 89. Bao hilo kwa Duchu ni la kwanza kwenye ligi msimu huu.

Mchezo huo umeifanya Simba kuchukua alama nne kwa Azam FC katika msimu huu wa 2023/2024 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Hata hivyo licha ya kushinda mchezo huo, Simba inasalia katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi ikiwa na pointi 56 iliyozivuna kwenye mechi 25 huku Azam ikibaki nafasi ya pili ikikusanya pointi 57 ikicheza mchi 26.

Ushindi wa Simba unamaanisha kwamba kama itafanikiwa kushinda mechi zake tano zilizosalia basi itamaliza ligi msimu huu juu ya Azam na kujikatia tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement