Yanga imefuzu hatua ya robo fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Belouizdad huku Simba ikihitaji ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya Jwaneng Galaxy iweze kusonga mbele, ilhali zote zimepewa waamuzi waliochezesha Afcon 2023.

Ijumaa, Machi Mosi, Yanga itakuwa ugenini jijini Cairo, Misri kukabiliana na Al Ahly kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, ikihitaji ushindi ili imalize ikiwa kinara wa kundi D ikiwa na pointi 11.

Jumamosi, Machi 02, Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kucheza na Jwaneng Galaxy ikihitaji ushindi ambao utaifanya ijihakikishie nafasi ya pili kwenye kundi B na kutinga robo fainali, ikiwa na pointi nane.


Mechi kati ya Al Ahly na Yanga itachezeshwa na refa Djindo Houngnandande kutoka Benin, wakati mchezo wa Simba na Jwaneng Galaxy utakuwa chini ya usimamizi wa refa Daniel Nii Laryea kutoka Ghana.

Refa Houngnandande kutoka Benin anakumbukwa na Yanga kwa kuchezesha mechi yao ya ugenini kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Monastir, Desemba 12 mwaka jana ambayo wenyeji waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, lakini pia alichezesha mchezo wa Kombe la Mataifa Afrika kati ya Zambia na Tanzania, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 nchini Ivory Coast.

Kwa upande wa Laryea, amewahi kuchezesha mechi moja ya Simba ambayo ilikuwa ni ya ugenini dhidi ya RS Berkane kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Februari 27, 2022 ambayo Simba ilipoteza kwa mabao 2-0 lakini pia kwenye michuano ya Afcon 2023, alichezesha mchezo kati ya Tunisia na Mali.

Marefa hao wawili wamekuwa pia na tabia ya kutovumilia rafu na matendo ya utovu wa nidhamu na pale yanapofanyika wamekuwa hawasiti kuonyesha kadi kwa wachezaji waliofanya, hii ikiwa ni alamu kwa Sadio Kanoute wa Simba na Khalid Aucho kwa upande wa Yanga.

Refa Laryea mwenye umri wa miaka 36, katika mechi 21 za mashindano ya klabu Afrika ambazo amechezesha, ametoa kadi 79. Nyekundu ni tatu na njano ni 76. Kwa upande wa Houngnandande (36), amechezesha idadi ya mechi 14 za mashindano ya klabu Afrika. Ameonyesha idadi ya kadi 59, mbili nyekundu na 57 zikiwa za njano.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement