Shirikisho la Soka la nchini Cameroon “FECAFOOT” limeeleza mshangao wake mkubwa baada ya wizara ya michezo ya nchi hiyo kumteua Marc Brys kuwa kocha mkuu mpya wa Kikosi cha Timu ya taifa hilo “Indomitable Lions”.

Kocha huyo Raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 61, ambaye hivi majuzi alikuwa OH Leuven inayoshiriki Jupiler Pro League ya nchini Ubelgiji amechaguliwa kuchukua nafasi ya mlinzi wa zamani wa Liverpool na West Ham Rigobert Song.

Hata hivyo, Fecafoot ambayo ipo chini ya Mshambulizi wa zamani wa Barcelona, Inter Milan na Chelsea Samuel Eto'o ilionekana kutojua juu ya uteuzi huo na kusema wazi kuwa uamuzi huo ulifanyika kwa upande mmoja.

Mshambulizi wa zamani wa Cameroon Francois Omam-Biyik, ambaye alishiriki katika Fainali tatu za Kombe la Dunia, ni miongoni mwa wafanyikazi walioongezwa katika benchi la ufundi la Timu hiyo ya Taifa huku Wizara ya michezo ikiweka wazi kuwa Brys atasaidiwa na Joachim Mununga na Giannis Xilouris.

Song aliteuliwa kuwa bosi wa Cameroon mwaka 2022 kwa amri ya Rais wa nchi hiyo, Paul Biya, lakini mkataba wake ulikamilika mwishoni mwa Februari mwaka huu.

Song aliiongoza Indomitable Lions kwenye Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, ambapo waliwafunga mabingwa mara tano wa Brazil na kutolewa katika hatua ya makundi huku mapema mwaka huu, akiondolewa kwenye Michuano ya AFCON2023 katika hatua ya 16 bora.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement