SAMATTA NA JOB WATEMWA KIKOSI CHA TAIFA STARS
NAHODHA wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Mbwana Samatta na Dickson Job wameachwa nje ya kikosi kitakachokwenda Azerbaijan kushiriki michuano mipya ya kirafiki ya FIFA SERIES 2024.
FIFA Series ni michuano mipya ya kirafiki ya mwaliko inayoandaliwa na FIFA inayohusisha timu za taifa ambazo zitacheza mechi za kirafiki dhidi ya timu kutoka mabara tofauti, na itafanyika mwezi Machi wa kila mwaka ambao unagawanyika kwa namba mbili. Mwezi huu wa 2024 ndio yanafanyika kwa mara ya kwanza.
Michuano hiyo itazileta pamoja timu za taifa za wanaume katika mfululizo wa michuano midogo inayohusisha timu za kutoka mashirikisho ya soka ya mabara sita yanayosimamiwa na FIFA. Kila kundi litakuwa na timu nne na michuano itafanyika katika kituo kimoja ikitumia muda wa mapumziko ya ligi ya kupisha mechi za kimataifa.