Usemi wa 'fuata nyuki ule asali unaweza kutumika vyema kumuelezea kocha kipenzi cha mashabiki na wadau wengi wa soka barani Afrika, Rulani Mokwena ambaye hivi karibuni ameiongoza Mamelodi Sundowns kutwaa ubingwa wa mashindano ya African Football League (AFL) ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika.

Ukaribu na imani iliyojengwa kwake na kocha mwenye jina kubwa Afrika, Pitso Mosimane hapana shaka umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio na heshima ambayo Mokwena mwenye umri wa miaka 36 hivi sasa anapata katika kazi ya kufundisha huku akifundisha kati ya timu bora zaidi barani Afrika, Mamelodi Sundowns. Mosimane ndiye mtu aliyekiona kipaji cha ukocha cha Rulani Mokwena na kumpendekeza awe miongoni mwa wasaidizi wake wakati huo akiinoa
Mamelodi na hilo lilifanyika mwaka 2014 wakati huo Mokwena akiwa na umri wa miaka 26 tu.

Mwaka 2017, Mokwena aliamua kutafuta changamnoto mpya katika timu ya Orlando Pirates ambako alienda kuwa kocha msaidizi wa Milutin Sredojevic 'Michơ' na baadaye Josef Zinnbauer lakini Machi, 2020 aliachana nayo na kutimkia Chippa United
ambayo ilimchukua awe kocha mkuu na Juni mkataba wake ulifikia tamati na ghafla akaibukia Mamelodi Sundowns ambayo ilimrudisha baada ya Mosimane kujiunga na Al Ahly.

Baada ya hapo, Mokwena ameliongoza jahazi la Sundowns hadi leo hii ambapo amekuwa akiimbwa Afrika nzima akisaidiwa kwa ukaribu na Manqoba Mngqithi.

Inawezekana kuzaliwa na kukulia katika familia ya soka kumechangia kwa kiasi kikubwa kumshawishi na kumhamasisha Mokwena kujituma hadi kufikia katika daraja alilonalo leo hii. Babu yake Eric 'Scara' Sono alikuwa nahodha wa Orlando Pirates, timu ambayo baba yake mzazi, Julius Sono pia aliichezea na kuishabikia.

Baba yake mkubwa ni nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana' na klabu za Orlando Pirates na New York Cosmos, Jomo Sono ambaye baadaye alikuja kuwa kocha msaidizi wa Afrika Kusini na kumiliki timu ya Jomo Cosmos.

Achana na taji la AFL ambalo ni kubwa zaidi kwa Mokwena kulitwaa tangu alipoanza kuwa kocha mkuu wa Mamelodi Sundowns, kocha huyo ameonyesha ubabe katika ligi ya ndani ambayo katika miaka mitatu aliyoitumikia ameonekana kukosa mpinzani.

Mokwena ametwaa taji la Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia 2020/2021 hadi msimu uliopita na anaelekea kutwaa taji la nne la ligi hiyo kwani timu yake ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 24, mbili zaidi ya zile za Supersport inayoshika nafasi ya pili ingawa
Mamelodi Sundowns yenyewe imecheza mechi mbili pungufu Chini yake, Mamelodi imetwaa taji moja la Nedbank na pia ina kombe moja la MTN 8.

Kazi yake nzuri imemfanya Mokwena kuwa miongoni mwa makocha wanaolipwa kiasi kikubwa cha fedha katika ngazi ya klabu huko Afrika Kusini ambapo anashika nafasi ya pili nyuma ya Mngqithi. Inaripotiwa kwamba kocha huyo analipwa kiasi cha Dola 49,561 ambacho ni zaidi ya Sh124 milioni kwa mwezi.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement