RS Berkane ya Morocco imefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali dhidi ya USMA ya Algeria kufutwa kwa mara ya pili ndani ya wiki moja.

Licha ya uwepo wa USMA kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, wachezaji hawakutoka kwenye chumba chao cha kubadilishia nguo kisha timu ikarudi kwenye basi lao na kuondoka uwanjani.

Mechi ya kwanza ya nusu fainali kati ya RS Berkane na wapinzani wa Algeria USM Alger tayari ilikuwa imekumbwa na matatizo.

Mechi hiyo ilifutwa kutokana na mzozo wa jezi za kuchezea nchini Algeria, na kusababisha RS Berkane kuzawadiwa ushindi wa mabao 3-0.

Mzozo uliibuka wakati timu ya Morocco ilipowasili Algeria kabla ya mkondo wa kwanza wa sare.

Maafisa wa forodha walikamata jezi za Berkane kutokana na kujumuishwa kwa ramani ya Morocco inayoonyesha Sahara Magharibi inayozozaniwa.

Sahara Magharibi inayozozaniwa, koloni la zamani la Uhispania, iko chini ya udhibiti wa Morocco lakini inadaiwa na Polisario Front inayoungwa mkono na Algeria, ambayo inatetea uhuru wa eneo hilo.

Suala hilo kwa muda mrefu limechochea mvutano kati ya mataifa jirani ya Algeria na Morocco.

RS Berkane sasa watawakaribisha Zamalek katika mchezo wa mkondo wa kwanza Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa nchini Morocco kabla ya ule wa marudiano utakaofanyika mjini Cairo.

Zamalek ilitinga fainali kwa kuwashinda Dreams FC ya Ghana kwa ushindi wa mabao 3-0 katika hatua ya nusu fainali.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement