ROBERT LEWANDOWSKI HUENDA AKAKOSA FAINALI YA EURO 2024 KUTOKANA NA MAJERAHA
Mshambuliaji wa Poland, Robert Lewandowski huenda akakosa fainali ya Euro 2024 kutokana na kuwa majeruhi.
Awali, fowadi huyo wa Barcelona aliripotiwa kwamba hatakuwapo kwenye mechi ya kwanza ya Poland kwenye fainali hizo zitakazofanyika Ujerumani kuanzia kesho Ijumaa, lakini sasa wasiwasi huenda asicheze kabisa mikikimikiki hiyo.
Lewandowski aliumia kwenye mechi ya kirafiki ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Uturuki, ambapo alipata maumivu ya paja yaliyomfanya ashindwe kumaliza mchezo huo. Na sasa kinachoelezwa, fowadi huyo veterani anaweza kukosa mechi ya kwanza ya Kundi D dhidi ya Uholanzi.
Ikiwa bado siku chache kwa fainali hizo, daktari wa Poland, Jacek Jaroszewski aliweka wazi uwezekano wa Lewandowski kukosekana kabisa.
Daktari huyo alisema: “Robert Lewandowski amepata matatizo ya misuli, ambayo itamfanya akose mechi ya kwanza ya michuano hii. Tunapambana kwa kadri tunavyoweza ili Robert aweze kucheza mechi ya pili dhidi ya Austria.”
Taarifa hizo ni pigo kubwa kwa Poland. Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 35 amefunga mabao 82 katika mechi 150 alizochezea timu ya taifa tangu mwaka 2008.
Wakati ikithibitishwa atakosa mechi ya kwanza, ripoti zaidi zinadai anaweza kukosekana kwenye fainali zote, huku fowadi mwenzake pia kwenye kikosi cha Poland, Karol Swiderski, naye alipata maumivu ya enka kwenye mechi dhidi ya Uturuki na hivyo kuzidisha presha.