REKODI ZA UGENINI ZA WYDAD ZINAIBEBA SIMBA
Wakati kocha Abdelhak Benchikha akisisitiza mechi ya leo ni sawa na fainali kwao, rekodi za Wydad kwenye mechi 10 za karibuni ugenini zinafufua matumaini kwa Simba kupata pointi tatu zitazowapa nguvu mpya kwenye msimamo katika kundi lake.
Simba inayocheza nyumbani kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni, kama itashinda itafikisha pointi tano na kupanda kwenye msimamo wa kundi B. Hadi sasa, katika msimamo wa kundi hilo, ASEC inaongoza ikiwa na pointi saba, Jwaneng Galaxy (4) na Wydad (3), Simba ni ya mwisho ikiwa na pointi mbili ilizovuna kwenye mechi tatu, ilifungwa moja na kutoka sare mara mbili.
Kama itashinda leo, itafikisha pointi tano huku ikiiombea kipigo Jwaneng Galaxy inayocheza na ASEC leo, maombi yao yakitiki, Simba itapanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo ikisikilizia matokeo ya mechi zake mbili zitakazosalia.
Mchezo wa leo ni wa kufa au kupona kwa timu hiyo kongwe ya soka nchini ambao kocha Benchikha anautaja kama mchezo wa fainali kwao. Kocha huyo amesisitiza kutokuwa na wasiwasi na pointi tatu, akibainisha wachezaji wake wanajiamini na kazi iliyobaki ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ambayo yatawaweka kwenye hali nzuri katika kundi lao.
"Hii (Wydad) ni timu kubwa lakini tulishacheza nao na ulikuwa mchezo mzuri, kwa sasa wana kocha mpya, namfahamu ni rafiki yangu na ni kocha mkubwa lakini hilo halitupi shaka kupata pointi tatu, tunajiamini," alisisitiza Benchikha.
Alisema kwenye mechi hiyo atawakosa wachezaji wawili kwenye eneo la kiungo, lakini bado sio tatizo kwenye kikosi chake, akirudia kusisitiza wanajiamini hasa baada mechi ya awali na Wydad nchini Morocco.
Kwa mara ya kwanza, Simba iliichapa Wydad bao 1-0 Aprili 22 nyumbani katika mechi ya robo fainali msimu wa 2022/23.
Kwenye marudiano nchini Morocco ilifungwa bao 1-0 na kwenda kwenye penalti ikatolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3. Kipigo kikubwa ambacho imewahi kukipata kutoka kwa timu hiyo ni cha Mei 28, 2011 Simba ilipofungwa mabao 3-0 nchini Morocco.
Licha ya matokeo hayo, bado rekodi za mechi za ugenini za Wydad zinaibeba Simba leo kutokana na historia ya kutofanya vizuri inapocheza nje ya Morroco.
Kipa wa Wydad, Youssef El Motie amekiri kwa miaka ya karibuni timu yao haina rekodi bora wakicheza ugenini, lakini hilo haliwasumbui kwani licha ya rekodi hiyo bado wamekuwa wakichukua mataji. Alisema jambo muhimu kwao ni kuhakikisha wanapata pointi tatu, leo akibainisha mabadiliko ya kocha sio tatizo kwao kwani wote wanaujuzi. Hata hivyo bado rekodi za ugenini za Wydad zinaibeba Simba kama itaamua 'kukaza' kwani katika mechi 10 kwenye Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho na za dunia za kirafiki za klabu, imefungwa tano, sare nne na kushinda mechi moja dhidi ya Enyimba (1-0 Oktoba 22).
Imefungwa na ASEC Mimosas 1-0, Mamelodi Sandowns 2-0, Al Hilal 2-1 mara mbili (Aprili 6 na Agosti 2) na kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Simba. Imepata sare ya bao 1-1 na Esperance Tunis na Hafia, ika-suluhu na Al Sadd na sare nyingine ya mabao 2-2 na Mamelodi Sundowns. Japo kocha, Faouzi Benzarti wa Wydad anaamini watafanya vizuri lakini dakika 90 za nguvu ndizo zitaamua matokeo. "Tupo tayari kupambana ndani ya dakika 90, kila mmnoja najua anataka ushindi kwenye mnchezo huu hivyo utakuwa mgumu, lengo letu ni kushinda,"alisema Benzarti.
Mbali na rekodi hizo, pia matokeo ya misimu mitatu iliyopita bado yanaipa nguvu Simba ya kufanya vizuri na kurejea rekodi yao kwenye mashindano ya kimataifa.
Nahodha Simba, Mohamed Hussein "Tshabalala' alisema wanafahamu umuhimu wa mchezo huo kwani na ni fainali kwao na watashuka uwanjani bila kujali matokeo ya mchezo uliopita. "Sisi kama wachezaji hatuna presha yoyote ile, ni kweli tupo nafasi ya mwisho kwenye kundi letu lakini tunafahamu tukipata matokeo basi yatafufua matumaini kwenye nafasi ya kuendelea kwetu'alisema.
Baadhi ya makocha nchini wanaamini Simba ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri endapo tu itatumia vema nafasi itakazopata. Wamekwenda mbali zaidi wakisisitiza Wydad ya sasa sio tishio kama ile ya miaka kadhaa nyuma, inafungika na kwa kuthibitisha hilo, wamebainisha hata Simba imewahi kuifunga na ikishinda leo itakuwa ni muendelezo tu.
"Kikubwa ni kutumia kila nafasi wanayoipata, wapate bao la mapema ambalo litawavuruga wapinzani, wasiruhusu pia kufungwa," alisema Charles Mkwassa kocha wa zamani wa timu ya taifa.