Refa Beida Dahane ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika kusimamia teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR) katika mechi ya kwanza ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Esperance na Al Ahly itakayochezwa Tunis, Tunisia, Mei 18.

Jina la Dahane limekuwa maarufu nchini tangu alipochezesha mechi ya marudiano baina ya Mamelodi Sundowns na Yanga iliyochezwa Pretoria, Afrika Kusini, Aprili 5.

Katika mechi hiyo, Dahane alitoa uamuzi uliozua mjadala baada ya kutoamuru mpira uliopigwa na Stephane Aziz Ki kuwa bao licha ya kuonekana ulivuka mstari na kuingia golini.

Katika mechi hiyo ya kwanza ya fainali, refa wa kati atakuwa ni Mustapha Ghobal kutoka Algeria.

Katika uteuzi huo wa Caf, mechi ya marudiano ambayo imepangwa kuchezwa jijini, Cairo, Mei 25, refa wa kati atakuwa ni Jean Jacques Ndala kutoka DR Congo.

Mwamuzi ambaye atasimamia VAR katika mechi ya marudiano ya hatua ya fainali atakuwa ni Benbrahim Lahlou kutoka Algeria.

Ikumbukwe pia Dahane ni miongoni mwa marefa 12 wa Afrika ambao watachezesha Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Ufaransa kuanzia Julai 26 hadi Agosti 11.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement