RAIS SAMIA SULUHU AONGEZA HAMASA ZAIDI KWA SIMBA NA YANGA KWA KUONGEZA DAU LA KILA GOLI MOJA KATIKA MICHUANO YA KLABU BINGWA AFRIKA
Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza hamasa kwa Klabu za Yanga na Simba kwenye mechi zao za robo fainali katika mashindano ya Kimataifa ya Klabu Bingwa Afrika ambapo atakuwa anatoa Tsh. milioni 10 kwa kila goli litakalofungwa kutoka Tsh. milioni 5 aliyokuwa anatoa katika hatua ya makundi.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema hayo leo March 20,2024 alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu (TPBL) na Wawakilishi kutoka Klabu za Simba na Yanga ili kujadili masuala mbalimbali kuhusu maendeleo ya michezo hapa Nchini na kuweka mikakati ya Klabu za Tanzania zinazoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika kufanya vizuri katika michuano hiyo.
Ndumbaro amesema “Mnaona kabisa Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza dau hilo ili timu zetu mbili ziweze kufanya vizuri na zipate mafanikio zaidi, tumeziambia timu zote mbili zishirikiane na Serikali katika kipindi hiki ili kupata mafanikio kwahiyo timu mbili zitakwenda kujipanga watasema wanahitaji Serikali ifanye nini ili kuhakikisha zinafanya vizuri kwa upande wa Serikali tuko tayari, uwanja uko tayari, masuala yote ya kiusalama yako tayari, maandalizi ya tiketi yako tayari na masuala mengine ambayo ni muhimu kwa Serikali kuyafanya ili mechi hizo ziwe kufanyika vizuri “
Simba inatarajiwa kucheza dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo utakaopigwa March 29,2024 huku Yanga akijiandaa kuvaana na Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini katika mchezo utafanyika March 30,2024 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dare es salaam.