Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Simba ijipange kwaajili ya msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutolewa kwenye robo fainali ya michuano hiyo na bingwa mtetezi Al Ahly leo kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri

Rais Samia ameandika kwenye mitandao yake ya kijamii “chezo mzuri Simba. Usiku haukuwa wa ushindi lakini tumeziona juhudi na zinatupa faraja na matarajio kuwa, msimu ujao wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa ya Shirikisho la Soka Afrika mambo yatakuwa mazuri zaidi. Ahadi yetu ni kuendelea kuwaunga mkono na kuwapa motisha.”

Simba imeishia Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara ya nne katika misimu sita baada ya kupokea kichapo cha jumla ya mabao 3-0 na Al Ahly bingwa mtetezi wa michuano hiyo.

Simba imepoteza ugenini mabao 2-0 Cairo yakifungwa Amr El Solia dakika ya 47 na Mahmoud Kahraba kwa penalti dakika ya 90 huku bao la kwanza lilifungwa na Ahmed Nabil Koka Machi 29, katika Uwanja wa Mkapa.

Pia Rais Samia Suluhu Hassan ameipa ujumbe Yanga baada ya kutolewa kwenye robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundowns kwa mikwaju ya penalti leo Afrika Kusini.

Rais Samia ameandika kwenye mitandao yake ya kijamii “Mchezo mzuri Yanga. Mmeonesha kiu na juhudi ya kuiletea heshima nchi yetu hadi kufikia hatua hii. Tunatarajia makubwa zaidi kutoka kwenu kwenye mashindano haya (Ligi ya Mabingwa ya Shirikisho la Soka Afrika) msimu ujao. Tutaendelea kuwaunga mkono na kuwapa motisha.”

Yanga imetupwa nje kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Mamelodi baada ya mechi kumalizika kwa suluhu ya 0-0 katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria, Afrika Kusini.

Yanga wamekosa penalti tatu zilizopigwa na Stephane Aziz KI, Dickson Job na Ibrahim Bacca na waliofunga ni Joseph Guede na Augustine Okrah huku Mamelodi zikipigwa na Marcelo Allende, Lucas Ribeiro Costa na Neo Maema na aliyekosa ni Gaston Sirino.







You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement