RAIS SAMIA AKIPOKEA KOMBE LA UBINGWA CECAFA U-15
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza Mabaraza ya Michezo kuendelea kuratibu na kufuatilia utendaji wa vyama vya michezo na kuhakikisha vinaendeshwa na kujiendesha kwa manufaa ya taifa.
Rais Samia amesema serikali inapoweka mazingira mazuri katika sekta ya michezo hutoa hamasa kwa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo kwa kuwekeza katika timu za vijana.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati wa hafla ya chakula cha mchana aliyoiandaa kuwapongeza wachezaji na viongozi wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 (Karume Boys) iliyofanyika Ikulu ndogo ya Tunguu.
Timu ya Karume Boys imetwaa Kombe la Mashindano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaliyofanyika nchini Uganda ambapo tangu miaka ya 1990 Zanzibar haijawahi kushinda katika mashindano hayo.
Vile vile Rais Samia amesema michezo hutoa fursa ya ajira kwa makundi mbalimbali hususan vijana hivyo viongozi hawana budi kuweka mipango endelevu na kuwekeza katika sekta hiyo.
Aidha, Rais Samia ameyataka Mashirikisho ya Soka Tanzania bara na Zanzibar kutumia mapato yanayotokana na viingilio vya mechi kufanya ukarabati wa viwanja badala ya kusubiri matengenezo makubwa ambayo yanaongeza gharama maradufu.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kutoa msukumo mkubwa katika kukuza sekta ya michezo nchini ikiwemo kurudisha ligi ya Muungano.
Zuhura Yunus Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,