BAO pekee la kipindi cha kwanza lililofungwa na Niclas Fulkrug lilitosha kuipa Borussia Dortmund ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Paris Saint-Germain kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa uliopigwa Signal Iduna Park usiku wa Jumatano.

Fulkrug alifunga bao hilo kwenye dakika 36 kufuatia asisti ya beki Nico Schlotterbeck na kuwapa mashabiki 81,365 waliokuwa wamejitokeza uwanjani hapo kushuhudia mubashara mchezo huo.



Kocha wa Dortmund, Edin Terzic alianza na fomesheni ya 4-2-3-1 na kumwaanzisha winga Jadon Sancho, anayecheza kwa mkopo akitokea Manchester United, timu yake ilimiliki mpira kwa asilimia 46, ikipiga mashuti manne yaliyolenga goli na matano yaliyopita pembeni huku kipa wake akifanya sevu tatu kuokoa hatari kufanya ushindi wao kuwa salama.

Upande wa PSG, kocha wao Luis Enrique, aliendelea kutamba na mfumo wake pendwa wa 4-3-3, huku Kylian Mbappe akiwamo kwenye chama lililoanza, alitawala mchezo kwa asilimia 54 licha ya kupoteza ugenini.

PSG ilipiga mashuti matatu yaliyolenga goli, huku 10 yakipita pembeni.

Miamba hiyo itarudiana Jumanne ijayo huko Ufaransa, ambapo mshindi atapata fursa ya kutinga fainali ambayo atamenyana na ama Real Madrid au Bayern Munich kwenye mchezo utakaopigwa Uwanja wa Wembley, Juni Mosi.






You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement