PHIRI APASHA MOTO VICHWA VYA MAKOCHA SIMBA
Moses Phiri amefunga mabao matatu katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji, Singida na Ihefu akitokea benchi.
Makocha wamesema, Robertinho anatakiwa kumuanzisha mshambuliaji Moses Phiri kamna anataka matokeo chanya kikosini haswa kwenye dabi ya Jumapili.
Phiri mwenye rekodi ya kucheza dakika 157, katika mechi sita za ligi mpaka sasa na amefunga mabao matatu katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji, Singida na Ihefu akitokea benchi.
Kocha Jamhuri Kihwelo Juliơ' ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba, alisema hakuna tatizo kwenye maamuzi ya Robertinho kumuingiza Phiri kwani Simba inapata matokeo hivyo bado maamuzi yake ni sahihi, ingawa anaamini akipata muda zaidi anaweza kufanya mambo makubwa.
"Mashabiki wanatakiwa kuelewa kuwa siyo wakati wote kocha atafanya wanachotaka hasa hawa wakigeni kikubwa ni Simba ina matokeo na sio Phiri kucheza kwani jambo la muhimu ni matokeo mazuri tu, ingawa kwa maoni yangu naamini akipata muda zaidi atafanya mambo makubwa.
"Kocha hawezi kuwa na chuki nabmchezaji wake anayempa matokeo mazuri, hivyo ni jambo la kusubiri tu tuone kwenye dabi itakavyokuwa," alisema Kihwelo ambaye ni Kocha wa zamani wa Simba na Taifa Stars.
Meja Abdul Mingange ambaye amewahi kuifundisha Mbeya City, alisema Robertinho yuko sahihi kwenye maamuzi ya kumtumia Phiri kutokana na kocha huyo ndiye anayewajua wachezaji wote wa Simba uwezo wao kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi.
Mingange alisema kocha huyo raia wa Brazil hawezi kukataa uwezo wa mchezaji aliye bora ambapo hatua ya kumtumia kwake kwa kumuingiza kipindi cha pili kinatokana na tathimini yake anavyomuona mazoezini.
"Shida kubwa hapa Tanzania watu hatujui kuheshimu taaluma za watu, Robertinho yupo Simba kama kocha wa kigeni na anajua anaifundisha timu yenye presha ya aina gani hawezi kupuuza ubora wa mchezaji ambaye anaweza kumpa matokeo,'alisema Mingange.
"Kesi kama hii imewahi kutokea pale Chelsea wakati kocha akiwa Mourinho (Jose) na alipokuwa anatofautiana na mmiliki wa klabu kutaka Shevchenko(Andrea) apewe muda wa kutosha lakini kocha alisimama na msimamo wake hakuyumba.
"Inawezekana mashabiki wa Simba wanavyotaka acheze kwa kuanza Phiri asingeweza kuonyesha kikubwa ambacho anakionyesha wakati anaingia kipindi cha pili, wote hatujui huko mazoezini amekuwa na kiwango Cha namna gani,nafikiri kwa kuwa timu inapata matokeo mashabiki wamuachie kocha afanye kazi yake."
Kocha Juma Pondamali aliyewahi kuitumikia timu ya Mashujaa, alisema; "Kumuingiza Phiri maana yake ni kwamba anataka kuusoma mchezo ili kupata matokeo mazuri na kuwadhuru wapinzani. Timu zilizoendelea huwa zikicheza ugenini haziwachezeshi wachezaji tegemeo ili wawasome wapinzani na wanapokuwa nyumbani wanawatumia ili kushambulia na kupata matokeo kwani hakuna mbinu mpya," alisema