PHIL FODEN AJIANDAA NA MPANGO WA KUWA MCHEZAJI MWINGEREZA ANAYELIPWA PESA NYINGI ZAIDI
Phil Foden anajiandaa na mpango wa kufanywa mchezaji Mwingereza anayelipwa pesa nyingi zaidi wakati atakaporejea kwenye klabu yake ya Manchester City akitokea kwenye majukumu ya kuitumikia England katika fainali za Euro 2024 huko Ujerumani.
Man City imeamua kukilinda kipaji chao hicho kwa kukipandisha msha-hara karibu mara mbili na hivyo sasa atakuwa akipokea kati ya Pauni 375,000 hadi Pauni 400,000 kwa wiki. Foden bado ana mkataba wa mi-aka mitatu kwenye kikosi hicho cha Etihad, lakini atakuwa na maisha matamu zaidi baada ya dili jipya.
Klabu kadhaa zilianza kuonyesha dhamira ya kuhitaji huduma ya mchezaji huyo ikiwamo mabingwa mara 15 wa Ulaya, Real Madrid.
Foden, 24, amepokea bonasi ya Pauni 200,000, lakini mshahara wake mpya utapanda na kufikia kiwango wanacholipwa wababe wengine kwenye kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola, Erling Haaland na Kevin De Bruyne.
Foden, ambaye aliibukia kutoka kwenye akademia ya Man City alikuwa na mchango mkubwa kwa msimu uliopita wakati alipoisaidia timu yake kushinda ubingwa wa nne mfululizo wa Ligi Kuu England, huku yeye akichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo. Dili hilo jipya litamfanya Foden kubaki kwenye kikosi cha Man City hadi atakapotimiza umri wa miaka 30.
Foden tayari ameshashida mataji 15, lakini anachotaka ni kuvunja rekodi ya Ryan Giggs ya kubeba mataji ya Ligi Kuu England mara 13.