Phil Foden amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa England kwenye tuzo zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Soka huko England.

Kiungo huyo mshambuliaji wa Manchester City amefunga mabao 24 na kuisaidia timu yake kuwa kwenye wakati mzuri wa kutetea mataji yake iliyobeba msimu uliopita, Ligi Kuu England na Kombe la FA.

Kwa kiwango chake bora cha msimu huu, kimeonekana na wajumbe wa FWA na kumchagua kuwa mchezaji bora wa mwaka kwa jumla ya kura asilimia 42.

Mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya England, Declan Rice, ambaye pia amekuwa na kiwango bora huko Arsenal, amechaguliwa kwenye nafasi ya pili, wakati staa mwingine anayecheza na Foden kwenye kikosi cha Man City, Rodri ambaye hajapoteza mechi yoyote kwa klabu yake katika kipindi cha miezi 15, ameshika nafasi ya tatu.

Nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard, fowadi wa Aston Villa, Ollie Watkins na kiungo mchezeshaji wa Chelsea, Cole Palmer wamekamilisha Sita Bora kwenye mchakamchaka huo wa tuzo za waandishi.

Lakini, Foden ni mchezaji wa tatu kutoka Etihad kushinda tuzo ya FWA kwa miaka ya karibuni baada ya Ruben Dias mwaka 2021 na Erling Haaland msimu uliopita.

Foden alisema: “Kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa waandishi ni heshima kubwa. Nimefurahi sana kupokea tuzo hii na nisiweza kupata kama si msaada kutoka kwa wachezaji wenzangu. Tuna kikosi bora kabisa na hakika ni bahati kubwa kuwa kwenye kundi hili la wachezaji.

“Nataka kuwashukuru wachezaji wenzake na Pep na makocha wengine kwa sapoti na ushauri ambao wamekuwa wakinipatia.”







You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement