OUSMANE DEMBÉLÉ, ASHINDA TUZO YAKE YA KWANZA YA BALLON D’OR
Ousmane Dembélé, mshambulizi wa Paris Saint-Germain, ameandika historia kwa kushinda tuzo yake ya kwanza ya Ballon d’Or mwaka 2025, akitangazwa rasmi katika sherehe zilizofanyika jijini Paris. Nyota huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 28 alihitimisha msimu uliopita akiwa na mafanikio makubwa, ambapo alicheza michezo 53 na kufunga mabao 35 huku akitoa pasi 14 za mabao, mchango uliosaidia PSG kushinda mataji makubwa yakiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu ya Ufaransa na Kombe la Ufaransa.
Dembele pia alikuwa miongoni mwa wafungaji bora wa Ligi 1, akiibuka na rekodi ya mabao 21, na akapewa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Safari yake ilimfikisha mbali zaidi baada ya PSG kutinga fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia, ingawa walipoteza kwa Chelsea. Tuzo ya Ballon d’Or ilimuweka mbele ya chipukizi wa Barcelona, Lamine Yamal, ambaye alimaliza nafasi ya pili, huku kiungo wa PSG, Vitinha, akimaliza wa tatu.
Wakati wa kupokea tuzo hiyo, Dembele alijikuta akitokwa na machozi ya furaha mbele ya hadhira kubwa, akishukuru familia yake, mashabiki na klabu ya PSG kwa kumsaidia katika safari yake ya mafanikio. Aliueleza ushindi huo kuwa si wa kibinafsi pekee, bali ni ishara ya nguvu ya timu nzima. Alisisitiza kuwa shinikizo la kushinda tuzo hiyo lilikuwa kubwa, na akasema kupokea kombe hilo kutoka kwa Ronaldinho, gwiji wa zamani wa PSG na Barcelona, ni tukio la kipekee lisiloweza kusahaulika.
Dembele alimshukuru rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi, na benchi la ufundi kwa kumsaidia katika kila hatua, akiwafananisha na familia. Pia alieleza kuwa wachezaji wenzake walimsaidia katika nyakati nzuri na ngumu, na hivyo mafanikio haya yanaonyesha mshikamano wa kikosi kizima cha PSG.



