ONANA ARUDISHA MATUMAINI KWA MASHABIKI WA SIMBA
Willy Onana amerejesha furaha kwa mashabiki wa Simba baada ya kuifungia timu yake bao la ushindi ikiichapa Coastal Union mabao 2-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Onana, aliyeingizwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Saido Ntibazonkiza, alitumia dakika tano tu ndani ya uwanja kufunga bao hilo la ushindi kwa ustadi mkubwa.
Katika mchezo huo, Simba ilitangulia kufunga kupitia kwa Freddy Michael kwenye dakika 11 baada ya mpira wa kona iliyochongwa na kiungo fundi wa mpira, Clatous Chama.
Hata hivyo, Coastal United ilisawazisha bao hilo dakika 14 baadaye, kupitia kwa Lucas Kikoti, aliyechopu mpira uliomzidi uwezo kipa wa Simba, Ayoub Lakred na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimefunga bao 1-1.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi 39, saba nyuma ya vinara Yanga yenye pointi 6, huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 17. Pointi hizo za Simba zinawafanya washike nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, huku Azam FC ikiwa ya pili baada ya kukusanya pointi 44 baada ya kushuka uwanjani mara 20.