NYOTA WA ZAMANI WA NIGERIA BABANGIDA AMEPATA AJALI YA GARI NA KUMPOTEZA MDOGO WAKE IBRAHIM BABANGIDA
Nyota wa zamani wa Nigeria na Rais wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa nchini humo (PFAN), Tijani Babangida amehusika katika ajali ya gari iliyotokea Alhamisi mchana iliyopelekea kifo cha mdogo wake, Ibrahim Babangida papo hapo.
Mshindi huyo wa medali ya dhahabu kwenye michuano ya Olimpiki ya Atlanta 1996, ambaye alisemekana kuwa ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo aligonga trela iliyokuwa ikitembea kando ya Barabara ya Kaduna Zaria wakati ajali hiyo ilipotokea.
Mchezaji mwenzake wa zamani, Emmanuel Babayaro, ambaye ni Katibu Mkuu wa PFAN, alifichua tukio hilo katika taarifa yake iliyosema "Ndugu! Tuwe katika maombi kwa ajili ya rais wetu, Tijani Babangida, ambaye ndiyo kwanza amepata ajali mbaya ya gari kwenye Barabara ya Kaduna-Zaria.
“Ibrahim Babangida, mdogo wake alifariki papo hapo kutokana na ajali hiyo huku Bw Rais (Babangida) na familia yake wakipelekwa hospitalini. Mungu ailaze roho ya Ibrahim Babangida kwa Amani,” alisema
Babayaro ambaye alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo alisema, "Ndiyo ni kweli. Ajali hiyo ilitokea walipokuwa wakielekea Zaria kutoka Kaduna”