NYASI BANDIA KUONDOLEWA UWANJA WA AMAAN ZANZIBAR
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay amesema Uwanja wa Amaan Zanzibar ni moja ya viwanja vitatu vitakavyotumika kwa ajili ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, lakini zile nyasi bandia zitaondolewa na kupandwa nyasi asilia ili ukidhi vigezo vya michuano hiyo ya kimataifa.
“Uwanja wa Amaan ushakamilika kwa asilimia 100. Kilichobaki ni kubadili tu zile nyasi bandia na kupanda nyasi asilia, jambo ambalo linachukua muda mfupi tu wa kuanzia,” amesema.
Viwanja vingine vya AFCON ni Benjamin Mkapa na mwingine mpya utakaoanza kujengwa mwezi Machi Arusha utakaochukua watu 30,000.”
Ameongeza: “Watu wengi wanazungumzia kuhusu viwanja vya mechi tu. Timu zitakuwa na viwanja vya wazi kwa ajili ya mazoezi ambavyo zinaweza kufanya mazoezi muda wowote, timu inakabidhiwa uwanja wake wa mazoezi na inaweza kufanya mazoezi muda wowote itakaotaka iwe mchana au usiku.
“Kwa Zanzibar vipo na vinaendelea kuandaliwa. Arusha maeneo ya wazi yapo. Kwa Dar es Salaam kuna Gymkhana, JK Park na hata Leaders Club pata tengenezwa kukidhi viwango vinavyohitajika ikiwa ni pamoja na kuwekewa taa.”
Amesema hayo jana Februari 14, 2024 wakati akichangia mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Ltd, wenye mada isemayo "Tanzania imejifunza nini kupitia AFCON 2023.