Mchezaji kinda wa Kitanzania, Shafii Omary ameanza kuimbwa huko Uturuki ambako anacheza soka la kulipwa baada ya kutupia bao moja na kutoa asisti ya bao jingine katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Silivrispor U19 wakati timu yake ya vijana Tuzlaspor ikiwasha moto licha ya kuwa pungufu kwa wachezaji wawili ambao walionyeshwa kadi nyekundu.

Shafii amehusika kwenye zaidi ya mabao 12 ya chama hilo ambalo vijana wamekuwa wakinolewa ikiwa ni hatua moja kabla ya kuanza kutumika kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Kinda huyo ambaye ni zao la taasisi ya African Youth Empowerment (AYE), alisema hakika ni faraja kwake kuona mashabiki wa timu hiyo wakiliimba jina lake na kwa upande mwingine inamfanya kuona ana kazi kubwa zaidi ya kufanya ili kuendelea kuwaaminisha kuhusu uwezo wake.

"Mechi ilikuwa ngumu sana kwetu maana tulikuwa pungufu lakini namshukuru Mungu kwa sababu alitusaidia na kushinda, kila mchezaji ilitubidi kujitoa zaidi ya kawaida na ilikuwa furaha ya kipekee kwangu kufunga bao la ushindi na kutoa asisti," alisema na kuongeza; "Mashabiki wa Tuzlaspor wamenionyesha upendo mkubwa sana, hakuna mchezaji ambaye nimeona amekuwa akiimbwa uwanjani, nilishangaa sana na kujituma zaidi hadi kufunga bao la ushindi, ambacho natakiwa kufanya ni kuendelea kujituma kwa sababu nipo hapa kwa ajili ya kutafuta njia zaidi za mafanikio kwenye safari yangu ya mpira."

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement