NDOTO ZILIZOMNYIMA USINGIZI NYOTA WA KIMATAIFA CRISTIANO RONALDO
BADO namfikiria yule mhenga aliyewahi kusema ng'ombe wa maskini hazai, bado najaribu kufikiria alikuwa anamaanisha ni ng'ombe halisia au alikuwa anazungumza kwa mafumbo. Bado najaribu kumfikiria yule mhenga.
Natamani kusema alikosa cha kuzungumza, pengine mimi ningekuwa naishi katika nyakati za wahenga, ningekuwa mtu wa kwanza kupinga baadhi misemo yao, kwa sababu huwa inashindwa kuishi katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu.
Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Ningeweza kupinga misemo hii kama ningekuwa na Cristiano Ronaldo ambaye ni mwakilishi mkuu wa kundi hili la ng'ombe wa maskini, kila mtu anamtazama Cristiano Ronaldo kama daraja la kwenda ng'ambo ya mafanikio.
Huwa namtazama Ronaldo kisha naitazama Madeira, kisha naitazama Ureno inavyoliimba jina lake, nawatazama watoto wanaojiita a.k.a za Cristiano Ronaldo lakini wasijue njia ambazo amezipitia shujaa huyu.
Natamani siku moja nimualike Cristiano Ronaldo azungumze na watoto na vijana awape mbinu sahihi ambazo zitawafanya wao waamini kwenye mafanikio lazima uteseke.
Natamani aje awaambie, aliye juu usimngoje chini ila ufanye kila namna uweze kumfikia, kwani huwezi kujua ni lini atashuka chini, au huko juu ndipo alipojitengenezea makazi yake.
Mtamuelewa vipi siku akiwaambia mama yake mzazi alishawahi kuwaza kutoa mimba yake kwa jinsi maisha yalivyokuwa magumu, je mtamuelewa akiwaambia kuwa alishawahi kulala chumba kimoja na dada zake?
Vipi mngemuonea huruma kama angewaambia alivyokuwa na miaka 14 alifanyiwa upasuaji wa moyo au mngetoa machozi kama angewaambia kuwa 2003, pombe ilimuondoa baba yake duniani?
Achana na kukulia katika mazingira ya kiparokia pale Funchal lakini mawazo yake yalikuwa yanawaza mpira, alikuwa anasahau hata kula chakula alikuwa anawaza mpira tu, ulikuwa ni utaratibu wake wa kutorokea dirishani na kuacha kazi alizokuwa anaachiwa na mwalimu wake wa kiroho Fernao Sousa.
Hata yeye anakumbuka kipindi kile akina Paul Scholes na Ryan Giggs walivyomshangaa alivyosema ipo siku atakuja kuwa mchezaji bora duniani, alitoa kauli ya kishujaa sana.
Bado atakumbuka siku yake ya kwanza kutangazwa kama mshindi wa tuzo ya mchezaji bora duniani, penginr hata baba yake Jose angekuwa anasafiri na mkewe kipenzi Maria kwenda kumtazama mwanae akibeba tuzo 5 za Ballon d'Or.
Bado nazitazama rekodi zake pale Old Trafford, naangalia mabao yake pale Santiago Bernabeu, staili yake ya kushangilia pale Turin, sichoki kuzitama Hat tricks zake akiwa na Ureno huku nikiona avyotangaza bidhaa zake pale Instagram.
Cristiano anaishi katika nukuu ya mwanafalsafa, Walt Disney ambayo alisema 'The way of getting start is quit talking and being doing'.
Wacha sisi tuendelee kuishi, tunamtazama Ronaldo wetu ana miaka 39 lakini bado anatamba pale Saudi Arabia
Kwa msimu huu tu wa 2023/2024 amefunga magoli 52 kwenye mechi 52 bila kusahu ameweka record ya kufunga hat trick 66