Mwanasiasa mkongwe wa Ujerumani ameomba radhi kwa jinsi alivyotoa maoni yake kuhusu rangi ya ngozi ya wachezaji wa timu ya soka ya nchi hiyo, ambapo aliwasifu na kwa kusema ingekuwaje iwapo kungekuwa na wachezaji weupe pekee.

Mbunge kutoka chama cha Greens, Katrin Göring-Eckardt, ambaye pia ni naibu kiongozi wa bunge la shirikisho la Ujerumani, alionekana kurejelea uchunguzi wa hivi karibuni uliogundua asilimia 21 ya waliohojiwa walipendelea kuona wazungu wengi zaidi katika kikosi cha Ujerumani.

"Timu hii ni ya kipekee. Hebu fikiria kama kungekuwa na wachezaji weupe wa Ujerumani pekee," aliandika baada ya Ujerumani kuifunga Hungary 2-0 katika michuano ya Euro 2024.

Lakini baada ya ukosoaji kwenye mitandao ya kijamii, wakiwemo wabunge wenzake, Bi Göring-Eckardt alifuta kauli yake na kuomba radhi.

Baadaye alienda kwenye ukurasa wa X, zamani Twitter, tena ili kujieleza. "Ilinisikitisha kwamba 21% ya Wajerumani walipendelea kuwepo "wazungu" zaidi katika timu ya taifa," Bi Göring-Eckardt aliandika.

"Ninajivunia timu hii na ninatumai kuwa tunaweza kuwashawishi 21% pia." Chapisho la awali la Bi Göring-Eckardt lilikosolewa haraka, huku wengine wakimshutumu kwa ubaguzi wa rangi licha ya ukweli kwamba alikuwa akisifu utofauti wa timu.

"Ninapata wasiwasi sana wakati watu nchini Ujerumani wanahukumiwa kwa rangi ya ngozi zao," alisema Wolfgang Kubicki, naibu kiongozi wa chama cha Free Democratic Party (FDP), ambacho ni sehemu ya serikali ya mseto ya Ujerumani pamoja na Greens.

Manuel Ostermann kutoka chama cha mrengo wa kati cha Christian Democratic Union (CDU) pia alitoa maoni. "Je, unawahukumu watu kulingana na sura zao? Kulingana na ufafanuzi wako mwenyewe, huo ni ubaguzi," alisema.

Utafiti huo ambao Bi Göring-Eckardt alikuwa akijibu uliidhinishwa na Sport Inside, ambayo inapeperushwa na shirika la utangazaji la Ujerumani WDR. Ilikuwa ni sehemu ya makala kuhusu tofauti za rangi ndani ya timu ya taifa na jinsi inavyotazamwa na umma.

Mchezaji Joshua Kimmich aliutaja uchunguzi huo kuwa wa "kibaguzi" uliporipotiwa kwa mara ya kwanza mapema mwezi huu, huku kocha Julian Nagelsmann akisema ulikuwa "wazimu".

"Tunacheza Euro kwa kila mtu nchini na yeyote anayecheza kandanda ya juu anaalikwa kuwa mchezaji wa timu ya taifa," Bw Nagelsmann alisema. "Natumai sitalazimika kusoma kura za uwongo kama hizi tena."

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement