MWANARIADHA WA KENYA AVUNJA REKODI YAKE YA DUNIA
Faith Kipyegon Mwanariadha kutoka nchini Kenya amevunja rekodi yake ya dunia katika mbio za Mita 1,500 za wanawake za Diamond League mjini Paris mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kipyegon alimaliza kwa saa 3:49.04, na kuipita rekodi yake ya 3:49.11, ambayo iliwekwa nchini Italia mwaka jana.
"Nilijua rekodi ya dunia iliwezekana kwa sababu hivi majuzi nilikimbia kwa kasi sana nchini Kenya," alisema Kipyegon, ambaye alitumia 3:53.98 katika Majaribio ya Olimpiki ya Kenya. "Nilikuwa nakuja hapa kukimbia mbio zangu tu na kuona nipo sura gani kutetea taji langu kwenye Olimpiki."
Wakimbiaji wengine tisa katika mbio hizo walipata matokeo bora ya kibinafsi. Jessica Hull wa Australia alimaliza wa pili kwa 3:50.83, akivunja rekodi yake ya Oceania kwa sekunde tano. Laura Muir alikuwa wa tatu katika rekodi ya Uingereza ya 3:53.79.
Kipyegon mwenye umri wa miaka 30 ameshinda medali ya dhahabu mara mbili ya Olimpiki katika mbio za Mita 1,500, baada ya kushinda mbio za Rio de Janeiro mwaka wa 2016 na Tokyo 2021.
Kabla ya Jumapili, alikuwa amekimbia mara mbili pekee mwaka wa 2024, katika Mbio za Mita 1,500 na 5,000, hadi kupata nafasi yake kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris katika majaribio ya Kenya mnamo mwezi Juni.
Utendaji wa Kipyegon ulikuja chini ya saa moja baada ya Yaroslava Mahuchikh wa Ukraine kuvunja rekodi ya dunia ya kuruka juu kwa kuruka Mita 2.10.