Wimbi la wanamichezo kufungiwa kutokana na matumizi ya dawa za zilizopigwa marufuku michezoni limeendelea kushika kasi kwa wanamichezo wa Afrika ambapo Mwanariadha kutoka nchini Ethiopia Zerfe Wondemagegn ambaye alifika fainali ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, na kukosa kidogo kuchukua Ubingwa wa dunia mwaka jana, amepigwa marufuku kwa miaka mitano baada ya kukutwa na dawa mbili zilizopigwa marufuku.


Zerfe amekiri kuvunja sheria za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli baada ya sampuli alizotoa kuashiria chembechembe za testosterone na nyinginezo ambazo zinaweza kusaidia damu ya mchezaji kusafirisha oksijeni zaidi.

Zerfe ambaye alishika nafasi ya nane katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka wa 2021 na wa nne katika mashindano ya dunia ya mwaka 2023 huko Budapest alichukuliwa sampuli mbili kati ya tatu katika kesi yake alipokuwa Hungary kwa hafla hiyo na ameondolewa kwenye mashindano.

Uamuzi wa AIU ulisema ulipokea ushuhuda wa barua pepe kutoka kwa daktari akisema Mwanamichezo huyo alipewa EPO kama dawa ya kutibu upungufu mkubwa wa damu na maambukizo ya figo lakini aliendelea na matumizi ya dawa hizo hivyo kukiuka sheria za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli. Shirika hilo liliongeza kuwa lilipokea idhini iliyotiwa saini kutoka kwa mwanariadha huyo wiki iliyopita.


Zerfe anakuwa mwanariadha wa hivi punde zaidi katika msururu wa visa vya matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwa wanariadha wa mbio ndefu ambapo Bingwa wa dunia wa mbio za kuruka viunzi kwa wanawake mwaka 2022, Norah Jeruto, anakabiliwa na kesi ya kusikilizwa kwa matumizi ya dawa za kusisimua misuli mwezi Juni, wiki tano kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Paris. 

Pia Jumatatu, AIU iliripoti kupigwa marufuku kwa miaka mitatu kwa mwanariadha Mkenya Celestine Chepchirchir, ambaye alipatikana na chembechembe za testosterone zikiashiria pia matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement