MUDATHIR YAHYA AFIKISHA MABAO 9 LIGI KUU BARA BAADA YA MCHEZO WA YANGA NA KAGERA SUGAR KUISHA KWA BAO 1-0
Licha ya nidhamu bora ya uzuiaji kwa Kagera Sugar ila imeshindwa kuizuia Yanga hadi dakika za mwisho baada ya kufungwa bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Bao la Yanga katika mchezo huo limefungwa na kiungo, Mudathir Yahya dakika ya 82 likiwa ni la tisa kwake katika Ligi Kuu Bara msimu huu akimfikia nyota wenzake, Maxi Mpia Nzengeli.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizi uliopigwa Uwanja wa Kaitaba Bukoba, Februari 2, mwaka huu uliisha kwa suluhu.
Yanga imeendeleza rekodi nzuri katika Ligi Kuu Bara inapocheza ikiwa uwanja wa nyumbani kwani haijapoteza wala kutoa sare tangu msimu huu wa 2023/2024 umeanza.
Huu unakuwa ni mchezo wa 13 kwa Yanga ikiwa mwenyeji na kati ya hiyo imeshinda yote sawa na kukusanya pointi 39 na imefunga jumla ya mabao 33 na kuruhusu matano tu.
Kwa upande wa michezo mingine 13 iliyocheza ya ugenini msimu huu, Yanga imeshinda tisa, sare miwili na kupoteza pia miwili na kati ya hiyo imefunga mabao 24 na kuruhusu saba sawa na kukusanya jumla ya pointi zake 29.
Ushindi huu unaifanya Yanga kufikisha pointi 68 katika michezo 26 iliyocheza, hivyo inahitaji pointi tano tu ili kufikisha 73 zitakazowapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kwa jumla tangu mwaka 1965 na kwa sababu hazitaweza kufikiwa na timu yoyote.