Timu ya Mtibwa Sugar imetoka suluhu na Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro jambo linalozidisha presha kuhakikisha inasalia kwenye ligi msimu ujao baada ya kuwa kwenye nafasi ya mwisho katika msimamo.

Mtibwa Sugar baada ya mchezo huo uliochezwa kuanzia saa 8:00 mchana imefikisha alama 21 ambapo imebakiwa na michezo miwili na endapo itashinda yote itaishia kuwa na alama 27 na ili ibaki Ligi Kuu au kucheza mtoano (play off) itapaswa kuziombea matokeo mabaya Geita Gold na Tabora United kwenye michezo iliyosalia.

Timu hiyo ilipanda Ligi Kuu 1995 ambapo msimu wa 1999-2000 ilitwaa ubingwa wa ligi na tangu wakati huo haikuwahi kushuka daraja ambapo ni miaka 29.

Mchezo mwingine uliochezwa leo wa Ligi Kuu ni ule uliwakutanisha Tanzania Prison na Mashujaa FC, Uwanja wa Sokoine umeendelea kuwa wa bahati kwa Mashujaa baada ya leo kuikanda mabao 2-1 Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara na kuongeza matumaini ya kubaki kwenye ligi.

Mashujaa iliingia uwanjani ikikumbuka kuchapwa mabao 2-0 na wapinzani hao walipokutana katika mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma na leo wamelipa kisasi.

Sokoine imeendelea kuwa neema kwa Mashujaa kwani wakati wanapanda Ligi Kuu Bara waling'ara kupitia uwanja huo walipoichapa Mbeya City bao 1-0 na kuishusha kupitia mchujo (play off).

Matokeo hayo yanaifanya Prisons kufikisha michezo tisa mfululizo bila ushindi ikiwa ni sare sita na kupoteza mitatu dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1, Ihefu 1-0 na leo kichapo hicho na kuwa nafasi ya sita kwa alama 33.

Mashujaa ambao ni msimu wao wa kwanza katika Ligi Kuu wanafikisha pointi 29 wakibaki nafasi ya 13 na sasa wanasubiri mechi mbili dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji kujua hatima yao kwenye ligi hiyo.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement