MSIMU WA PILI WA MASHINDANO YA GOFU SERIES YANATARAJIWA KUANZA JUNI 29 MKOANI ARUSHA
Msimu wa pili wa mashindano ya Gofu Series mkoani Arusha unatarajiwa kuanza Juni 29.
Mashindano hayo ambayo yalianza mwaka jana na kuhudhuriwa na wachezaji kutoka sehemu mbalimbali za nchi hii yanajulikana kama NCBA Bank Golf Series yakiwa yanalenga kukuza vipaji vya gofu pamoja na kutangaza shughuli za utalii.
Mashindano haya ni ya muendelezo na tayari ni mashindano makubwa sana na kivutio nchini Kenya, Uganda, na Rwanda.
Zaidi ya wacheza gofu 100 wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Arusha Gymkhana Golf Club.
Mmoja kati ya watu wa heshima watakaohudhuria ni Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Damas Ndumbaro, ambaye pia ni mchezaji mahiri wa gofu hapa nchini.
“Lengo la mashindano hayo si tu kusherehekea gofu bali pia ni jukwaa la kutambua na kukuza mabingwa wa baadaye ambapo pia Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo atakuwepo. Washindi watatu wa kipekee kutoka mashindano haya watapata nafasi ya kushiriki fainali zitakazofanyika Nairobi, Kenya,” alisema Claver Serumaga, Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Tanzania.