Baada ya wasiwasi juu ya majeraha ya pua aliyopata katika michuano ya Euro akiwa na Ufaransa, staa wa Real Madrid Kylian Mbappe anadaiwa kuwa anaendelea vizuri na anaweza kucheza katika mchezo wa Uefa Super Cup dhidi ya Atalanta.

Mbappe ambaye hakujumuishwa katika kikosi cha Madrid kilichosafiri kwenda Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu kwa ajili ya kuangaliza zaidi hali ya pua yake kwa sasa anaendelea vizuri na kocha wa Madrid, Carlo Ancelotti ameweka wazi kwamba anaweza kumtumia katika mchezo huo.

Tangu kumalizika kwa michuano ya Euro ambapo kapteni huyu wa Ufaransa na timu yake waliishia nusu fainali, Mbappe hajacheza mechi yoyote ya kimashindano.

Akizungumza na waandishi wa habari nchini Marekani, Ancelotti alisema:”Mbappe ni wazi anaweza kucheza Super Cup, Jude Bellingham (ambaye hayupo na timu katika maandalizi) na wengine wote pia wanaostahili kucheza watacheza.”

Kama ilivyo kwa Mbappe, Bellingham pia hakusafiri na timu kwenda Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya baada ya kupewa mapumziko kwa kuitumikia England katika michuano ya Euro 2023 ambapo walitinga fainali na kupoteza dhidi ya Hispania kwa kichapo cha mabao 2-1.

Real Madrid ambayo imepoteza mechi mbili za kirafiki ilizocheza katika maandalizi ya msimu dhidi ya AC Milan na Barcelona, inatarajiwa kushuka dimbani leo huko North Carolina itakapoumana na Chelsea.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement