Azam imemsainisha mkataba wa mwaka mmoja, mshambuliaji Adam Adam, ambaye msimu ulioisha alimaliza na mabao saba, akiwa na Mashujaa FC na muda wowote kuanzia sasa itamtambulisha rasmi.

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' imeelezwa ndiye aliyesimamia dili lake, ndani ya mkataba huo kukiwa na sharti moja.

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo aliliambia Mwanaspoti kwamba wamekubaliana na mchezaji huyo endapo akifanya vizuri watamuongeza mkataba mwingine na maslahi yake yatakuwa mazuri zaidi.

"Tumemalizana na Adam, kwa sasa ni mchezaji halali wa Azam, kocha ndiye aliyempendekeza baada ya kuo-nyesha kiwango kizuri msimu ulioisha, ameona ataongeza nguvu safu ya ushambuliaji," amesema.

Kiongozi huyo, amesema Adam ni kama karejea nyumbani, kwani alikuwapo katika kikosi B chao mwaka 2011-2014, alikuwa na kina Aishi Manula, Mudathir Yahya na wengine.

"Kocha aliyempandisha alikuwa Joseph Omog msimu wa 2014/15, lakini akatolewa kwa mkopo kwenda Lipuli kipindi hicho ilikuwa daraja la kwanza," amesema kiongozi huyo.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement