Kocha Arne Slot ameanza kazi Liverpool, lakini kibarua cha kwanza kinachomkabili ni sintofahamu ya hatima ya supastaa mwenye thamani ya Pauni 100 milioni, Mohamed Salah.

Staa Salah aliweka wazi mwezi uliopita kwamba atabaki Anfield kupambania mataji msimu ujao kitu ambacho kilimpa matumaini Slot, ambaye ametua kuchukua mikoba ya Jurgen Klopp.

Lakini, winga huyo wa kimataifa wa Misri amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake huko Anfield, hivyo kocha Slot na wamiliki wa klabu hiyo, Fenway Sports Group wanakuna vichwa kwa sasa, wampige bei staa huyo kwenye dirisha hili au wasubiri kumpoteza bure mwakani.

Salah ambaye amekuwa kinara wa mabao kwenye timu hiyo kwa misimu saba iliyopita, amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na miamba ya Saudi Pro League, Al-Ittihad.

Kutokana na Klopp kuondoka, Salah, 31, anafahamu wazi anaweza kubadili mshahara wake wa Pauni 19.5 milioni kwenda kuwa Pauni 375 milioni kwa miaka mitatu atakayosaini huko Saudia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Liverpool, Michael Edwards ni shabiki mkubwa wa Mo Salah, ambaye alisainiwa na Klopp kwa ada ya Pauni 34.3 milioni akitokea AS Roma mwaka 2017.

Endapo kama atakwenda Saudi Arabia atakwenda kukutana na mastaa wengine kibao akiwamo Cristiano Ronaldo, Karim Benzema na Neymar kwa kuwataja kwa uchache.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement