MICHUANO YA DAR PORT KAGAME CUP 2024 TIMU ZATAKIWA KUTUMIA NAFASI HIYO KAMA MAANDALIZI YA MSIMU UJAO WA KIMATAIFA
Klabu shiriki michuano ya Dar Port Kagame Cup 2024 zimetakiwa kutumia vizuri mashindano hayo kama sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano hususani mashindano ya Kimataifa.
Meneja wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Nchini “TFF” Baraka Kizuguto ameeleza kuwa mashindano hayo yatazidi kuziimarisha Klabu kwaajili ya mashindano mbalimbali yaliyo mbele yao.
Kwa Upande mwingine Kizuguto ameelezea mfumo mzima wa mashindano hayo yatakayoanza kutimua vumbi Julai 09 mpaka 21 katika Dimba la Chamazi sambamba na KMC uliopo Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam.
Michuano Hiyo itawakilishwa na Klabu 12 kutoka Mataifa tofauti ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama CECAFA
zikiwa zimegawanywa katika makundi matatu ambapo Kundi A limebeba timu ya Coastal Union ya Tanzania, Al Wadi ya Sudan, JKU ya Visiwani Zanzibar na Dekedaha ya nchini Somalia.
Al Hilal ya Sudan, Gor Mahia ya Kenya, Red Arrows ya Zambia na Djibout Telecom ya Djibout zenyewe zipo Kundi B huku Kundi C wakiwemo SC Villa ya Uganda, APR ya Rwanda Singida Big Stars ya Tanzania na El Mereikh ya Sudan Kusini.