MECHI 9 YANGA ILIZOKUTANA NA NAMUNGO IMESHINDA MARA 5
Mabingwa watetezi hao wanarudi uwanjani kuvaana na Namungo katika mechi ya ligi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, mjini Lindi, huku vijana wa Mwinyi Zahera wakipania kuweka rekodi mbele ya wababe hao.
Timu hizo zinapokutana huwa hakuna dakika 90 nyepesi, lakini Namungo haijawahi kuitambia Yanga licha ya kuibana mara kadhaa na kutoka nayo sare na leo imetamba inataka kufuta unyonge huo iliyonayo tangu ipande daraja mwaka 2020.
Yanga itashuka katika mchezo huo ikichekelea kutokana na matokeo waliyopata wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Simba waliochapwa 2-1 na Tanzania Prisons na Azam waliolazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Coastal Union, wakati wenyeji wakitoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC.
Matokeo hayo yataufanya mchezo wa Yanga utakaopigwa kuanzia saa 12:00 jioni kuwa wa presha kubwa ikitaka kurudi kileleni mwa msimamo ilikoshushwa juzi baada ya Azam ku-pata pointi moja.
Yanga inakumbuka kwamba mchezo dhidi ya Namungo uliopita ikiwa nyumbani ililazimika kushinda 1-0 jioni kwa bao la kiungo Mudathir Yahya pale Azam Complex.
Katika mechi 9 Yanga ilizokutana na Namungo imeshinda mara tano, huku nne zikisha kwa sare na hakuna mchezo ambao Namungo imeshinda.