SIKU moja baada ya ajali mbaya ya gari aliyoipata mchezaji wa zamani wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia, Rainford Kalaba, inadaiwa mwanamke aliyekuwa naye wakati ajali hiyo Charlene Mkandawire ni mke wa rafiki yake.

Vyanzo mbalimbali vya habari Zambia vimeripoti Mkandawire ndiye aliyekutwa kwenye kiti cha dereva baada ya gari ndogo aina ya Mercedes Benz aliyokuwa anaendesha kugongana na Lori la mafuta, jana Kafue, jijini Lusaka, Zambia.

Kwa mujibu wa ripoti Mkandawire alifariki dunia papo hapo huku Kalaba mwenye umri wa miaka 37, akiwahishwa hospitalini kupatiwa matibabu zaidi na hadi sasa hali yake bado ni mbaya.

Awali haikutambulika ni mwanamke gani aliyekuwamo kwenye gari hiyo hadi mapema hii leo zilipoibuka taarifa hizo kutoka Zambia.

Pia kumekuwa na video inayosambaa ikimwonyesha mwanamke huyo mrefu wa kimo akicheza muziki na kalaba.

Mkuu wa kitendo cha uhusiano wa nje wa University Teaching Hospital (UTH), huko Zambia amesema madaktari hospitalini hapo wanaendelea kufanya linalowezekana kuhakikisha mchezaji wa zamani wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia Rainford Kalaba anarudi katika hali yake.

Akizungumza akiwa Hosptalini hapo alisema "Hali yake sio nzuri na madaktari wetu wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anarudi katika hali yake, alipata ajali ya gari nafikiri kila mtu anafahamu hilo lakini tunapambana kadri tuwezavyo ili awe sawa na napenda kukanusha taarifa zinazotolewa na baadhi ya media kwamba amefariki, hapana ni mzima."

Kabla ya kustaafu soka Julai mwaka jana akiwa na Mazembe, Kalaba alikuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa timu hiyo akiisaidia kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2015.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement