MCHEZAJI WA ZAMANI WA KIMATAIFA CARLOS TEVEZ AMELAZWA HOSPITALI BAADA YA KUUMWA KIFUA
Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Argentina Carlos Tevez amelazwa hospitalini baada ya kuumwa na kifua.
Tevez alipelekwa hospitalini mjini Buenos Aires siku ya Jumanne na atasalia hapo hadi vipimo vya afya vikamilike.
Mshambulizi huyo wa zamani wa Manchester United, Manchester City na West Ham mwenye umri wa miaka 40 sasa ni kocha mkuu wa timu inayoshiriki ligi kuu ya Argentina Independiente
Independiente alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, kwamba vipimo vya awali vya Tevez katika Hospitali ya Trinidad huko San Isidro "vilikuwa vya kuridhisha" lakini atalazwa hapo kwa wakati huu kama "tahadhari".
Tevez, ambaye aliichezea Argentina mechi 76 kati ya 2004 na 2015, alichukua jukumu la kuinoa Independiente mnamo Agosti 2023.
Hapo awali alikuwa kwa muda mfupi Rosario Central, baada ya kustaafu kama mchezaji mnamo Juni 2022 baada ya kipindi cha tatu na Boca Juniors.
Tevez alicheza mechi 201 kwenye Ligi Kuu ya England kati ya 2006 na 2013 na kufunga mabao 84.
Alishinda taji la Ligi Kuu mara mbili akiwa na United (2007-08 na 2008-09) na mara moja akiwa na City (2011-12).