MASTAA WA KUCHUNGWA ZAIDI DARBY YA KARIAKOO
Joto na presha kubwa ni katika mchezo wa watani wa jadi Jumapili kutokana na namna ambavyo tỉmu zote kwa sasa zimekuwa na matokeo mazuri.
Yanga ndiye kinara kwenye Ligi ikiwa na pointi 18 katika mechi saba huku Simba ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 18 kwenye mechi sita ilizocheza. Simba msimu huu hadi sasa imefunga mabao 16 na kuruhusu mabao matano huku upanda wa Yanga yenyewe imefunga mabao 20 na kuruhusu nyavu zake zitikiswe mara nne. Katika mechi hizo wapo wachezaji ambao namba zao zinawabeba na wanatakiwa kuchungwa kwani kama wakiachiwa uwazi mdogo tu basi wanaweza kutoa matokeo mazuri kwa timu zao kwenye dabi.
JEAN BALEKE
Huyu ndiye kinara wa kufunga mabao katika kikosi cha Simba hadi sasa akiweka wavuni mabao sita. Ni mshambuliaji ambaye anaweza kutumia nafasi vizuri. Baleke licha ya kwamba ni mzuri wa kutumia nafasi lakini kubwa zaidi silaha inayombeba zaidi kwamba akiwa ndani ya eneo la hatari basi hakukosi kizembe. Mshambuliaji huyu amefunga mabao matano ndani ya eneo la hatari na moja nje ya boksi ni wazi kabisa anatakiwa achungwe asipate nafasi hizo ndani ya boksi.
Baleke mabao aliyofunga ndani ya boksi ni katika mechi tano tofauti dhidi ya Coastal Union (alifunga matatu), Dodoma Jiji (moja), Mtibwa Sugar (moja) huku kwenye mchezo dhidi ya Ihefu alifunga bao moja ambalo ni nje ya boksi. Safu ya ulinzi Yanga inabidi iwe makini kuhakikisha kwamba Baleke hawi huru kuingia ndani ya boksi lao.
STEPHEN AZIZ KI
Kwa upande wa Yanga yeye ndio kinara wa ufungaji akiweka wavuni mabao sita hadi sasa. Ni mshambuliaji ambaye ni ngumu kutabili muda gani anafunga. Mshambuliaji huyu ni hatari ndani na nje ya boksi kwani amefunga mabao matatu ndani ya boksi na matatu nje ya boksi.
Mtindo wake wa kufunga nje ya boksi katika nabao yake mawili ni kwa njia ya mipira ya adhabu (Free Kick) hivyo ni wazi Simba inabidi iwe makini kwenye kufanya makosa nje ya boksi lao. Aziz Ki amefunga mabao ndani ya boksi kwenye mechi ya Kmc (bao moja), Geita (bao moja) huku ya nje ikiwa dhidi ya JKT Tz (bao moja) na Azamn (mabao mawili).
SHOMARI KAPOMBE
Beki huyu ni wazi kabisa anatumika kwa kiasi kikubwa katika kupeleka mashambulizi ya Simba kutokana na spidi yake ndani ya uwanja. Kapombe amehusika kutoa pasi moja ya bao la Moses Phiri katika mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji. Jambo lingine beki huyu ni mzoefu wa kutosha na dabi hivyo hatokuwa katika uoga wowote ule ndani ya uwanja.
YAO ATTOHOULA
Ni beki mzuri ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga na kutoa pasi za mabao. Hadi sasa ametoa pasi za mabao nne na kufunga bao moja(dhidi ya JKT Tz) tu katika Ligi Kuu. Beki huyu anasifika kwa uwezo wake wa kupeleka mashambulizi na hilo lipo wazi kwani namba zake zinaonyesha wazi. Simba inabidi iwe makini na beki huyu kwani Yanga inamtumia hata kwenye ukabaji hivyo anaweza akapunguza spidi za mawinga wao kupeleka mashambulizi.
MOHAMED HUSSEIN 'TSHABALALA'
Kuna muda huwa anaonyesha kama vile amechoka hasa kurudi kukaba, hilo linatokana na namna ambavyo anakuwa anapeleka mashambulizi langoni kwa wapinzani. Tshabalala kwenye mabao sita ya Baleke ametoa pasi mbili za mabao kwenye mechi mbili tofauti ambazo ni dhidi ya Coastal Union na Dodoma Jiji. Hivyo ni wazi kabisa kwenye dabi hii ni mchezaji wa kuchungwa kutokana na uwezo wake wa kutoa pasi za mabao akitokea upande wa pembeni.
MAX ZENGELI
Ameingia vizuri kwenye mfumo wa Yanga kwani hadi sasa amefunga mabao matano na kutoa pasi za bao mbili kwa Aziz Ki. Kiungo mshambuliaji huyu pia ana uwezo wa kupeleka presha kubwa kwa wapinzani wake kutokana na spidi yake na umililki mkubwa wa mpira mguuni. Max pia ana sifa ya kulazimisha kuingia eneo ambalo hata kama ni gumu kuingilika kwani sio muoga wa mabeki wa upinzani.
MOSES PHIRI
Licha ya kwamba sio mchezaji wa kikosi cha kwanza kwa kocha Robertinho lakini ameonyesha hana masikhara anapopewa nafasi. Phiri kwenye mechi tatu tofauti alizocheza amefunga mabao matatu na kuonyesha wazi yeye sio mshambuliaji wa kawaida hata kama hapati nafasi. Kwa sasa ukimtoa Baleke ndani ya Simba mwenye mabao sita basi anafuata yeye mwenye matatu huku akiwa sio mchezaji anayepata nafasi ya kuanza. Ni wazi kama hatoanza kwenye mchezo huu basi anapoingia mabeki wa Yanga wanatakiwa wawe makini kuhakikisha hawapi madhara.