MASTAA 6 WA ARSENAL WALIOBADILISHWA VIWANGO NA MIKEL ARTETA
Declan Rice
Moja ya kati viungo ghali kwenye Ligi Kuu England, Declan Rice mwenyewe amekiri kiwango chake uwanjani kimebailika kwa kiasi kikubwa tangu alipotua Arsenal tofauti na alivyokuwa West Ham United.. Sawa, Rice alipokuwa West Ham United alifanikiwa kubeba moja kati ya mataji ya Ulaya, lakini anafichua jambo baada ya kutua Arsenal kwa uhamisho wa Pauni 105 milioni na kuwa chini ya Arteta.
"Ni wiki nne tu zimepita, lakini sasa najiona nimebadilika kisoka na kuwa mchezaji mwingine kabisa tofauti na nilivyokuwa awali," alisema Rice na kuongeza. "Hakika kwa sasa naitazama mechi kwenye namna tofauti kabisa. Kimbinu, nikiwa na mpira au nisipokuwa nao. Nafurahia nimejifunza mengi sana na naendelea kujifunza, kuna hatua kubwa nimepiga. Kuna vitu sikuwa navyo huko nyuma."
Martin 0degaard
Kocha Arteta anakubali mavitu ya kiungo mchezeshaji, Martin Odegaard na alizungumzia kufurahia kwake baada ya mkali huyo wa kimataifa wa Norway kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Arsenal. Kocha Arteta alisema, Arsenal inategemea mambo mengi na kwa miaka mingi kutoka kwa staa huyo wa zamani wa Real Madrid.
Lakini, Odegaard, ambaye ndiye nahodha wa Arsenal, naye alifunguka na kusema mipango madhubuti ya Arteta na namna anavyofundisha soka ndicho kitu kilichomvutia na kuamua kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki kwenye klabu hiyo ye Emirates. Staa huyo alidumu kwenye kikosi cha Real Madrid kwa miaka sita, lakini hakupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza na kujikuta akitolewa kwa mkopo mara kadhaa, kabla ya kutulizana Arsenal na maisha yamekuwa matamu chini ya Arteta, ambapo Odegaard wa sasa anaonekana kuwa tofauti na pengine hata Real Madrid watatamani arejee kwenye kikosi.
Gabriel Jesus
Mbrazili huyo alishinda mataji manne ya Ligi Kuu England na kufunga mabao 95 kwa kipindi chake cha miaka miaka mitano na nusu aliyokuwa Manchester City. Hata hivyo, staa huyo alionekana kama nyongeza tu kwenye kikosi hicho cha Man City ambacho kilisheheni mastaa wa maana wakati anacheza. Staa, Jesus mwenyewe alimntaja Arteta kwamba ndiye sababu iliyomfanya akajiunge na Arsenal, baada ya kufanya kazi kwa karibu na kocha huyo wakati walipokuwa pamoja Etihad.
Kiwango chake kimekuwa kikipanda na kushuka kutokana na kuwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini kwa nyakati ambazo anakuwa fiti, Jesus anakuwa kwenye ubora mkubwa kwelikweli kwenye kikosi cha Arsenal tofauti na alivyokuwa Man City. Arsenal inakuwa kwenye ubora mkubwa sana inapomtanguliza Jesus kwenye safu yake ya ushambuliaji, huku mchezaji huyo akionekana kuwa tofauti kabisa tangu alipoanza kuwa chini ya Kocha Arteta huko Emirates.
William Saliba
Unaweza kushangaa kwa sasa kwa sababu awali kulikuwa sintofahamu ya beki Saliba juu ya hatima yake kwenye kikosi cha Arsenal baada ya kuonekana kutokuwa vizuri na Kocha Arteta. Baada ya kusajiliwa na kisha kuachwa acheze kwa mkopo kwenye klabu za Saint Etienne, Nice na Marseille - hatimaye Saliba alivutwa Arsenal na kuanza
kupewa nafasi ya kucheza. Na tangu wakati huo, Kocha Arteta amemtengeneza Saliba na kumfanya awe miongoni mwa mabeki mahiri wanaoanza kufikiriwa kwenye wale waliobora kwenye Bara la Ulaya.
Kiwango bora cha soka lake chini ya Kocha Arteta kimemfanya beki huyo wa kati kusaini mkataba mpya wa miaka minne wa kucheza Arsenal hadi 2027 na sasa panga pangua amekuwa nguzo imara kwenye safu ya ulinzi ya miamba hiyo ya Emirates.
Aaron Ramsdale
Kocha Arteta wakati anamchukua kipa Aaron Ramsdale alizua maswali mengi kuhusu ubora wake wake kwa sababu huko alikotoka, alizishusha daraja mara mbili mfululizo alipokuwa na Bournemouth na Sheffield United. Kumbe Arteta alifahamu kitu gani anafanya na baada ya Ramsdale kutua tu kwenye kikosi chake alimbadili na kumfanya kuwa mmoja wa makipa matata sana kwenye Ligi Kuu England.
Msimu huu ameamua kumpa nafasi David Raya, lakini hilo haliondoi ukweli wa kile ambacho akilifanya kwa kipa Ramsdale na kumfanya kuwa gumzo kwa sasa huko England kwamba anastahili kuondoka kwenda kujiunga na timu nyingine kulinda kiwango chake kama Arsenal haimpi nafasi ya kucheza. Arsenal ilikuwa kwenye uwezo wa kuwa timu inayoweza kushindania ubingwa wakati Ramsdale alipokuwa kwenye goli lao msimu uliopita.
Leandro Trossard
Winga huyo wa Kibelgiji bado hajapata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal, lakini ni ingizo la maana kwelikweli kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Emirates. Licha ya kwamba amekuwa akitokea benchi, Trossard ameasisti mara 10 kwenye Ligi Kuu England katika nusu ya pili ya msimu wa 2022-23 ambapo timu hiyo ilikuwa ikifukuzia ubingwa.
Kiwango chake Arsenal, Trossard ana wastani wa bao au asisti moja kwa dakika 89 tangu alipoanza kuwa chini ya Arteta, wakati alipokuwa chini ya Roberto De Zerbi huko Brighton, mchango wake ulikuwa kila baada ya dakika ni 142, wakati chini ya Graham Potter alikuwa na wastani wa bao au asisti moja kwa kila dakika 236.