MAPINDUZI CUP KUANZA RASMI DESEMBA 28
Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 inatarajiwa kuanza rasmi Desemba 28 hadi Januari 13 kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Unguja.
Michuano hiyo kwa msimnu huu itashirikisha timu 12 nne kutoka Zanzibar, nne kutoka Tanzania Bara huku Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zikitoa timu moja moja. Timu hizo zitakazo shiriki michuano hiyo msimu huu kutoka Zanzibar ni bingwa mtetezi Mlandege FC, KVZ, Jamhuri na Chipukizi, wakati Bara ni Azam FC, Simba, Yanga na Singida Fountain Gate, URA kutoka Uganda, Bandari ya Kenya, Vital'O ya Burundi na APR ya Rwanda.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano hayo, Suleiman Mahmoud Jabir alisema michuano hiyo msimnu huu itakuwa mikubwa na yenye mvuto tofauti na misimu iliopita, ikiakisi miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema vigezo walivyovitumia kwa timu za Zanzibar ni kufanya droo na hawakuzingatia timu ambazo zipo nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo ipo kwenye mzunguko wa 14 kwa sasa.
"Hii droo ilitokea kama bahati nasibu tuliweka vikaratasi vya timu baadae tukachagua timu zilizobahatika ndio hizo tulizozijumuisha kwenye muichuano hiyo kwa msimu huu" alisema.
Alisema michuano hiyo itachezwa kwa hatua ya makundi ambapo kila kundi litakuwa na tỉmu nne, ukiachana na mchezo huo wa soka pia kutakuwa na mashindano mbalimbali kama vile resi za ngalawa, riadha na makachu.