MANCHESTER CITY KUFANYA MABORESHO KATIKA KIKOSI CHAKE MSIMU WA 2024/25
Baada ya kushinda mataji manne mfululizo kwenye Ligi Kuu England, Manchester City sasa inahitaji kufanya maboresho makubwa kwenye kikosi chake katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kuleta wachezaji wengine watakaokuwa na njaa ya mafanikio.
Kutokana na hilo, kuna mastaa wake wakubwa kabisa wataondoka kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, hivyo kocha Pep Guardiola na mabosi wake kwenye kikosi hicho cha Man City watahitaji kufanya usajili wa nguvu kufanya kikosi kuwa imara na chenye hamu ya kufanikiwa.
Kiungo mchezeshaji Kevin De Bruyne, mmoja kati ya wanasoka wenye historia ya kutosha kwenye kikosi cha Man City, lakini mkali huyo tayari ameanza kuvutiwa na ofa za pesa nyingi za kutoka klabu za Saudi Pro League.
De Bruyne, ambaye atatimiza umri wa miaka 33 wiki chache zijazo, alikosa miezi mitano ya kwanza msimu uliopita kutokana na maumivu ya misuli na kinachoonekana staa huyo anaweza kuachana na maisha ya Etihad baada ya kuwa kwenye kikosi hicho kwa miaka tisa.
Kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes, ambaye anauzwa Pauni 100 milioni, anatajwa kama mtu anayefaa kwenda kurithi buti za De Bruyne endapo kama ataondoka, huku wachezaji wengine akiwamo staa wa Bayern Munich, Jamal Musiala na Dani Olmo wa RB Leipzig wakiwa kwenye rada pia za miamba hiyo ya Etihad wakihitaji huduma zao wakakipige kwenye Ligi Kuu England.
Kipa wa Man City, Ederson naye yumo kwenye rada za klabu za Saudi Arabia baada ya miaka saba ya kuichezea timu hiyo. Majina mengine mawili makubwa kabisa kwenye kikosi cha Man City ambao wanaweza kufungasha virago vyao na kuondoka kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ni Jack Grealish na Bernardo Silva, jambo litakalomfanya kocha Guardiola kuhitaji kufanya uwekezaji mkubwa kwenye kikosi ili kuendeleza utawala.