Mafunzo ya kufunga vifaa vya kiteknolojia kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi kwamaana ya (VAR) yamefanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam yakiongozwa na Meneja wa Teknolojia ya Soka kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Wael Elsebaie.


Mafunzo hayo ya kuvifunga sambamba na kuviendesha vifaa hivyo yameshirikisha jumla ya watu sita ikiwemo Watanzania wane sambamba na Raia wa Kenya wawili.

Imewekwa wazi kuwa mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, yataanza mafunzo kwa Waamuzi waweze kutumia VAR katika michezo mbalimbali.


Kwa upande mwingine Mkufunzi wa Waamuzi kutoka Tanzania Leslie Liunda ameteuliwa na CAF kuhudhuria Kozi ya Wakufunzi wa VAR itakayofanyika Juni 24-27, 2024 Cairo nchini Misri.

Kwa ujumla wake hiyo ni moja ya matekelezo ya CAF sambamba na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ambapo mapema mwaka huu alieleza juu ya matumizi ya VAR katika mechi za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa msimu ujao.


Rais Karia aliweka wazi kuwa tayari walishapokea nyaraka kutoka CAF kwa ajili ya kupokea vifaa vya VAR, lakini kabla ya hapo kutakuwa na mafunzo kwa waamuzi ya namna ya kuvitumia ikiwa ni katika ule mpango wa CAF kusaidia 'zone'.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement