MABINGWA WATETEZI WA CAFCL AL AHLY WAMEFIKA KWA MKAPA MARA NNE NA KUONDOKA BILA USHINDI
Wakati Simba ikitaarajia kushuka Uwanja wa Mkapa leo saa 3:00 usiku kukipiga na Al Ahly katika mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, macho na masikio ya wengi yataelekezwa kwenye bato la beki wa kushoto wa Wekundu wa Msimbazi, Mohammed Husein 'Tshabalala' na winga wa kulia wa Mashetani Wekundu, Percy Tau.
Licha ya kuwa ni mechi ya kwanza kuwania kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu, lakini itakuwa ya heshima zaidi kutokana na rekodi za timu hizo mbili ambazo rangi yao asili ni nyekundu.
Simba ambao ni wenyeji imekuwa na rekodi bora inapokuwa katika Uwanja wa Mkapa kwa miaka ya hivi karibuni, kutokana na matokeo ambayo imekuwa ikiyapata.
Wekundu hao wa Msimbazi wamedhihirisha hilo hata mbele ya wapinzani wao wa leo Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo kwani wamefika kwa Mkapa mara nne jumla kucheza na Simba na mara zote wameondoka bila ushindi.