Bado nakumbuka maneno ya mama yangu mzazi ambayo mpaka sasa yapo kwenye kichwa changu, Mama yangu aliwahi kuniambia 'Mwanangu, heshimu mwanamke kwani anaweza kukushauri wema au ubaya'. 

Pengine wewe unaweza usinielewe, ila nikimfuta Luis Suarez pale Catalunya kwa sasa na kumwambia maneno haya atanielewa kwa uzuri huku akiniuliza natumia kinywaji gani, ni yeye pekee atakayenielewa.

Suarez atakumbuka kipindi kile anaishi mitaa ya kule Salto akiosha magari ili ajipatie pesa ya kulea familia, atakumbuka baba yake alivyoikimbia familia kutokana na vyuma kukaza, atakumbuka yeye mwenyewe alivyoanza ulevi na matumizi ya bangi kule mtaani, atakumbuka maisha yake ya enzi za kujitafuta yaivyokuwa yamejaa kila aina ya misukosuko.

Pia atakumbuka jinsi ambavyo hakuona umuhimu wa kipaji chake cha kucheza mpira wa miguu lakini alitokea mtu mmoja ambaye alimpa nguvu mpya ya kutafuta viatu vya kuanza kuonea nyavu za viwanja vya mtaani, huyu ni kama alitumwa kwa Suarez.

Unamjua Sofia Balbi? Sio mama yake, huyu ni rafiki mkubwa Antonella Roccuzzo na Daniella Fabregas, ni mke wa Luis Suarez. Pengine huwa unamuona tu ukafikiri labda alipenda pesa za Suarez anazozipata kutoka kwenye soka. Unakosea sana.

Mwanamama huyu alizaliwa pale Montevideo, mji mkuu wa Uruguay, Suarez yeye alizaliwa pale Salto. Kutoka Montevideo kwenda Salto sio mbali ni kilometa 1.8 tu, ukienda kwa gari ni dakika 5 na ukitumia miguu ni dakika 21. 

Huyu ndiye aliyekutana mtaani na Luis Suarez, akamwambia acha ujinga, sipendi tabia yako ya ulevi mimi ninachokitaka ukiendeleze hiki kipaji chako cha soka, kipindi hicho wamekutana na Sofia yeye alikuwa na miaka 15. Sofia akiwa na miaka 17 anaondoka Uruguay anakwenda Barcelona Hispania, anamuacha Suarez Uruguay.

Huyu Suarez ambaye amebatizwa jina la El Pistolero au The Gunman, amekuwa hivi kwa sababu ya mwanamke huyu ambaye alimshauri arudi kwenye soka kama kawaida kwani angepotea.

Kumbuka hapo mwanamke ameenda Barcelona, yeye yupo Uruguay hapo inabidi atumie siku moja na masaa 15. Hiyo haikuwa shida kwake, shida ni kwamba atafikaje? Hapo hakuona namna nyingine zaidi ya kupambania soka, imani yake kama mbegu ya haradali aliamini itamfikisha Hispania siku moja.

Mwaka 2006, lengo la kwanza lilikamilika. Lengo hilo lilikuwa ni kufika Ulaya, haijalishi ni wapi, ilimrada ni Ulaya. Alifika Uholanzi kwenye klabu ya Groningen, akakichafua sana, kwa mwaka tu, Ajax Amsterdam wakamchukua. Kilichotokea hapo, waholanzi wenyewe wanajua.

Januari 31 mwaka 2011, lengo la pili lilikamilika. Baada ya Fernando Torres kwenda Chelsea kwa mkwanja mrefu wanaziba pengo kwa kusajili washambuliaji wawili, Andy Carroll kutoka Newcastle kwa na Luis Suarez kutoka Ajax. 

Sipendi sana kukumbushia mauaji ambayo aliyafanya El Pistolero pale kwenye ardhi ya malkia, sitaki kukumbuka jinsi alivyofunga zile hat-trick pale Anfield na viwanja vingine kama hana akili nzuri. Safu ya ushambuliaji ya SSS aliiongoza yeye, yaani Suarez, Sturridge na Sterling.

Namtunuku Sophia Balbi vyeti binafsi kwa kile ambacho amekionesha El Pistolero.

Wakati watu wakimshutumu Suarez kwa tabia zake za kung'ata wachezaji wenzake, Sofia yeye anajua ni kawaida yake. Yeye amelelewa na mtaa, mtaa umemlea, ukitaka uhuni upo ndani yake. Ila kwa mtoto mzuri pale hana neno.

Tuwe na ndoto kama za Suarez, tutatoboa tu

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement