Ligi Kuu Zanzibar inahitimisha mzunguko wa 20 wikiendi hii, Bodi ya Ligi hiyo imefanya mabadiko ya tarehe kwa baadhi ya michezo.

Ligi hiyo itasimama kwa mwezi mmoja kupisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan baada ya mzunguko huo wa 20 kukamilika na Ligi Daraja la kwanza na Daraja la Pili Ngazi ya Mkoa.

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi, michezo hiyo ni timu ya Hard Rock dhidi ya Kipanga FC ambao ulitakiwa kuchezwa Februari 29, lakini ulichezwa jana Jumanne Februari 27 katika Uwanja wa FFU Finya - Pemba.

Pia mchezo kati ya timu ya Mafunzo FC dhidi ya JKU SC sasa utachezwa Jumapili ijayo, Machi 3 lakini awali ulitakiwa kupigwa Ijumaa, Machi Mosi huku mtanange kati ya Uhamiaji FC dhidi ya Jamhuri FC uliotakiwa kuchezwa Machi Machi 3 hivi sasa utapingwa Machi Mosi.

Kwa mujibu wa mabadiliko michezo mingine itachezwa kama ilivyopangwa ambapo mabingwa KMKM SC itacheza na Ngome FC katika Uwanja wa Mao A, huku Malindi dhidi ya Maendeleo United utachezwa katika uwanja wa Mao B Februari 29.

Majirani Dabi itachezwa Machi 2 kati ya Mlandenge dhidi ya Kundemba ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Mao A na Zimamoto dhidi ya KVZ wataminyana Machi 3.

Mzunguko wa 20 utamalizika Machi 3 kwa michezo miwili kuchezwa kati ya Mafunzo FC dhidi ya JKU SC na Zimamoto FC itaminyana na KVZ.

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Machi 4 mpaka 9 itachezwa michezo ya Kombe la FA hatua ya 32 bora.

daktari wa timu ya KMKM, Adam Juma kazungumzia kusimama kwa ligi kupisha mfungo, amesema imefanyika hivyo kutokana na imani ya dini ya Kiislamu visiwani Zanzibar.

“Hakuna athari yoyote (kiafya) kwa mchezaji kucheza ligi kukiwa na Mfungo wa Ramadhani, uamuzi wa kusimama kwa ligi ni kutokana na imani kubwa iliyopo hapa Zanzibar,”

“Lakini kwa namna nyingine kuna athari kwa timu zenyewe kutokana na kusimamishwa kucheza zikiwa tayari zimejijengea ushindani hadi wanarudi tena watatakiwa kuanza upya.”

Mbali na kusimama kwa Ligi Kuu Zanzibar, pia imezoeleka kila msimu wa mfungo wa Ramadhani, Ligi zingine pia husimamishwa.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement